********************
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma inatarajia ufaulu wa asilimia 100 kwa matokeo ya mtihani wa darasa la Nne kitaifa ulioanza leo nchi nzima.
Matarajio hayo yalitolewa na Mkuu wa Divisheni ya Elimu Msingi Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mwl. Prisca Myalla alipokuwa akielezea matarajio ya matokeo ya mtihani huo kwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Mwl. Prisca alisema kuwa lengo la ufaulu kwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma ni asilimia 100. “Hivyo, matarajio ya ufaulu yanaenda sambamba na lengo la ufaulu ambalo ni asilimia 100. Wanafunzi wetu wameandaliwa vizuri kitaaluma. Mwaka 2021, Halmashauri ilikuwa na ufaulu wa asilimia 94” alisema Mwl. Myalla.
Akiongelea idadi ya wanafunzi wanaofanya mtihani wa taifa wa darasa la Nne, alisema kuwa jumla ya watahiniwa 18,304 wanafanya mtihani huo. “Shule zinazofanya mtihani wa taifa wa darasa la nne katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma ni 144 kati ya shule 156 zilizopo katika halmashauri. Shule 144 zinazofanya mtihani wa sarasa la Nne za serikali ni 96 na binafsi ni 48” alisema Prisca.
Halmashauri ya Jiji la Dodoma ina jumla ya Kata 41 na mitaa 222.