Mkurugenzi Msaidizi wa Usalama Mtandao wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Stephen Wangwe akizungumza katika mafunzo ya usalama mtandao kwa Wanafunzi wa Taasisi ya Karume ya Sayansi na Teknolojia Zanzibar (KIST) leo Oktoba 25, 2022 .
Mkurugenzi Msaidizi wa Usalama Mtandao wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Stephen Wangwe akisisitiza jambo wakati wa mafunzo hayo.
Washiriki wakiwa kwenye mafunzo hayo.
Mafunzo yakitolewa.
………………………………………….
Na
Mwandishi wetu, WHMTH, Zanzibar.
WATANZANIA
wameshauriwa kuacha tabia ya kuchapisha picha na video za faragha mtandaoni kwa
kuwa ni kinyume na maadili ya kitanzania lakini pia mhusika anaweza kupata
madhara ya kisaikolojia kutokana na udhalilishaji anaoweza kuupata mtandaoni.
Mkurugenzi
Msaidizi wa Usalama Mtandao wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya
Habari, Mhandisi Stephen Wangwe amezungumza hayo wakati akitoa mafunzo ya
usalama mtandao kwa wanafunzi wa Taasisi ya Karume ya Sayansi na Teknolojia
Zanzibar (KIST) Oktoba 25, 2022 .
Amesema
kuwa, matukio ya picha na video za faragha mtandaoni yanazidi kuongezeka na
asilimia kubwa zinawekwa bila idhini ya wahusika baada ya kusalitiwa na watu
waliowaamini au baada ya kupoteza kifaa cha TEHAMA kilichohifadhi picha hizo.
“Tunapaswa
kufikiri kwanza kabla ya kupiga, kurekodi, kutuma na kusambaza matendo ya
faragha katika mtandao ili kulinda heshima binafsi na kulinda maadili ya
kitanzania”, amezungumza Mhandisi Wangwe
Ameongeza
kuwa Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015, inazungumza wazi kuwa
uchapishaji wa picha au video za faragha mtandaoni (ponography) ni kosa
kisheria na adhabu yake ni faini si chini ya milioni 20, au kifungo kisichopungua
miaka saba au vyote kwa pamoja.
Mhandisi
Wangwe ametoa rai kwa jamii kulinda faragha zao kwa kuhakikisha faragha inabaki
kuwa faragha lakini pia kuhakikisha wanalinda vifaa vyao vya TEHAMA kwa kuweka
password imara na ikiwezekana zaidi ya moja ili ikitokea kimepotea basi iwe
ngumu mtu kufungua au kuona kilichopo ndani.
Naye
Mtaalamu wa Usalama Mtandao, Bw. Yusuph Kileo amesema kuwa udhalilishaji wa
kimtandao unaongezeka katika jamii na madhara yake ni makubwa sana kwa wahusika
ikiwa ni pamoja na msongo wa mawazo au hata vifo hutokea.
“Ni
kosa kisheria kudhalilisha watu kwa njia ya mtandao na faini yake si chini ya
milioni tano, kifungo cha miaka mitatu au vyote kwa pamoja lakini pia ni muhimu
jamii kuhakikisha hatutengenezi mazingira ya kufanyiwa udhalilishaji
mtandaoni”, amesisitiza Kileo.
Rashidi Salim Abdallah , mwanafunzi wa TEHAMA wa Taasisi ya Karume ya Sayansi
na Teknolojia Zanzibar amesema kupitia mada zilizotolewa na wataalamu wa
usalama mtandao wamejifunza kujiuliza nini faida ya vitu wanavyoposti mtandaoni
na kuepuka vishawishi vya kuwaamini na kuwatumia picha za faragha watu
wanaokutana nao na kuanzisha mahusiano mtandaoni.
Imeandaliwa
na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara
ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.