Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi,Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako, akiwahutubia washiriki wa mafunzo ya usalama na afya yaliyoandaliwa na OSHA na kutolewa kwa Maafisa Rasilimali Watu, Maafisa Ununuzi na Ugavi, Wakaguzi wa Ndani na Maafisa Mipango kutoka katika Wizara, Mashirika ya Umma na Taasisi nyingine za Serikali. Waziri Ndalichako alikuwa anafungua mafunzo hayo ya siku mbili (Oktoba 25 na 26) yanayofanyika katika ukumbi wa OSHA jijini Dodoma.
Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi Khadija Mwenda, akitoa maelezo ya awali kwa washiriki wa mafunzo ya usalama na afya yaliyoandaliwa na OSHA na kutolewa kwa Maafisa Rasilimali Watu, Maafisa Ununuzi na Ugavi, Wakaguzi wa Ndani na Maafisa Mipango kutoka katika Wizara, Mashirika ya Umma na Taasisi nyingine za Serikali.
Mkurugenzi wa Mafunzo, Utafiti, Takwimu na Uhamasishaji wa OSHA, Bw. Joshua Matiko, akijibu hoja mbali mbali zilizoibuliwa na washiriki wa mafunzo ya usalama na afya mara baada ya kuwasilisha mada kuhusu usimamizi wa mifumo ya Usalama na Afya mahali pa kazi. Waliokaa kwenye meza kuu ni Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda (katikati) na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Sheria, Bi. Netiwe Mhando.
Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda (katikati), Mkurugenzi wa Mafunzo, Utafiti, Takwimu na Uhamasishaji wa OSHA, Bw. Joshua Matiko (kulia) na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Sheria, Bi. Netiwe Mhando (kushoto) wakiwasikiliza washiriki wa mafunzo ya usalama na afya mahali pa kazi yaliyoandaliwa na OSHA na kutolewa kwa Maafisa Rasilimali Watu, Maafisa Ununuzi na Ugavi, Wakaguzi wa Ndani na Maafisa Mipango kutoka katika Wizara, Mashirika ya Umma na Taasisi nyingine za Serikali.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya usalama na afya wakifuatilia mada mbali mbali zkatika mafunzo hayo yaliyoandaliwa na OSHA na kutolewa kwa Maafisi Rasilimali Watu, Maafisa Ununuzi na Ugavi, Wakaguzi wa Ndani na Maafisa Mipango kutoka katika Wizara, Mashirika ya Umma na Taasisi nyingine za Serikali. Mafunzo hayo yalifunguliwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Prof. Joyce Ndalichako.
*******************
Na Mwandishi Wetu
Wito umetolewa kwa wadau wa sekta ya umma kushirikiana kikamilifu na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) kuimarisha mifumo ya usalama na afya mahali pa kazi katika maofisi na miradi mbali mbali ya serikali.
Wito huo umetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako alipokuwa akifungua mafunzo maalum ya usalama na afya yaliyoandaliwa na OSHA na kutolewa kwa Maafisa ya Wizara, Mashirika ya Umma, Idara na Taasisi nyingine za serikali.
Maafisa walioalikwa kushiriki mafunzo hayo kwa awamu ya kwanza ni pamoja na Maafisa Rasilimali Watu na Utawala, Maafisa Ununuzi na Ugavi, Maafisa Sheria, Wakaguzi wa Ndani na Maafisa Mipango ambao kwa namna moja au nyingine wanahusika katika usimamizi wa Ofisi za Umma, mifumo mbali mbali ya kiutendaji pamoja na ustawi wa wafanyakazi.
Katika hotuba yake ya ufunguzi, Prof. Ndalichako, ameipongeza OSHA kwa kutekeleza maagizo ya Ofisi yake ambapo awali iliwaagiza kufanya ukaguzi katika ofisi zote za serikali na kisha kutoa mafunzo na ushauri wa kitaalam juu ya uboreshaji wa mazingira ya kazi katika ofisi hizo pamoja na miradi mbali mbali ya ujenzi inayoendelea.
“Ni matarajio yangu kwamba baada ya mafunzo haya ya siku mbili mtapata uelewa wa kutosha kuhusu Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi na mtaweza kwenda kuisimamia vizuri. Tunawaomba mkawe mabalozi wetu na mkatusaidie kuwaelekeza wafanyakazi wachukue tahadhari kwani mnaweza kuwapa vifaa vinavyotakiwa lakini wakavitumia tofauti na maelekezo ya kitaalam.
Aidha, niwapongeze OSHA kwa kutekeleza maagizo niliyowapatia mwezi Aprili lakini ningependa kuona mnawafikia wadau wengi zaidi na hata baadae mnaweza kupanga kuwakutanisha Makatibu Wakuu kwa ajili ya kuwapa elimu hii ili kurahisisha utekelezaji wa masuala haya,” ameeleza, Waziri Ndalichako.
Akizungumza wakati wa ufunguzi huo wa mafunzo, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda amesema mafunzo hayo ni sehemu ya mrejesho wa kampeni ya ukaguzi na uchunguzi wa afya za wafanyakazi uliyoendeshwa na Taasisi yake mwezi Aprili na kubaini changamoto mbali mbali za usalama na afya ikiwemo uelewa mdogo miongoni mwa wadau.
“Mafunzo haya ni sehemu ya mkakati wetu wa kushughulikia changamoto tulizozibaini katika zoezi tuliloliendesha mwezi Aprili ambapo tulibaini uwepo wa ombwe la uelewa na hivyo tumeamua kuliondoa kupitia mafunzo haya kwa makundi mbali mbali ya watumishi ambao tutawafikia kwa nyakati tofauti,” amesema Khadija Mwenda, Kiongozi Mkuu wa Taasisi ya OSHA.
Aidha, ameleza kuwa kupitia mafunzo hayo kutakuwa na uelewa wa pamoja miongoni mwa watendaji mbali mbali wa serikali na hivyo kuwezesha utoaji wa huduma kwa wananchi katika ofisi za umma pamoja miradi mbali mbali ya serikali kufanyika kwa kuzingatia kanuni za usalama na afya.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mafunzo, Utafiti, Takwimu na Uhamasishaji, Bw. Joshua Matiko, amesema programu hiyo imeandaliwa kwa lengo la kuondoa dhana iliyojengeka kwamba wafanyakazi katika maofisi hawakabiliwa na vihatarishi vya usalama na afya.
Washiriki wa mafunzo hayo ya siku mbili (2) wameelezea umuhimu wa mafunzo waliyoyapata.
“Ni mafunzo ambayo binafsi yamenijenga na yamenipa uelewa mkubwa hivyo yatanisaidia sana katika kazi zangu za kila siku lakini pia jambo ambalo nitalipeleka ofisini kwangu ni namna ambavyo tunapaswa kuhakikisha kwamba wakati wote tunajali usalama wa wafanyakazi wote na mambo mengine yatafuata,” ameeleza Bi. Rose Chipembele- Afisa Rasilimali Watu Wakala wa Taifa wa Uhifadhi wa Chakula (NFRA).
“Mafunzo haya mimi nimeyapokea kwa mwitikio mkubwa sana kwani nimejua hatari ambazo zinaweza kunikumba huko mbeleni endapo sitazingatia tahadhari zinazoshauriwa na wataalam. Tumeelezwa kwamba athari za magonjwa yatokanayo na kazi ni za muda mrefu pengine hata ukishakuwa umestaafu na matokeo yake unaweza kujikuta hata kile unachokipata baada ya utumishi wako unawezakuishia kukitumia kwa ajili ya matibabu,” ni maneno ya Bw. Stanley Jackson- Mkuu wa Kitengo cha Ununuzi na Ugavi-Mamlaka ya Rufaa za Zabuni za Umma (PPAA).
Mafunzo hayo yanayotolewa kwa siku mbili (Oktoba 25 hadi 26) katika ukumbi wa OSHA Dodoma yamewaleta pamoja Maafisa wa Serikali wanaohusika moja kwa moja katika uendeshaji wa Ofisi za Umma na Ustawi wa Wafanyakazi wakiwemo Maafisa Rasilimali Watu, Maafisa Ununuzi na Ugavi, Wakaguzi wa Ndani, Wanasheria pamoja na Maafisa Mipango. Lengo likiwa ni kuwajengea uelewa ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia utekelezaji wa masuala ya usalama na afya katika sehemu zao za kazi.