Julieth Laizer ,Arusha.
Arusha.Halmashauri ya jiji la Arusha imefanikiwa kukusanya mapato ya ndani zaidi ya sh 7.2 bilioni katika robo ya mwaka 2022/2023 tofauti na 2021/2022 ambapo walikusanya sh.6.2 bilioni sawa na ongezeko la sh.1.4 bilioni.
Akiongea na vyombo vya habari ofisini kwake wakati akitoa taarifa ya mapato ya robo ya mwaka 2022/2023,Meya wa jiji la Arusha,Maximilian Iranqhe amesema fedha hizo zimeelekezwa katika miradi ya maendeleo ikiwemo hospitali ya wilaya na ujenzi wa shule pamoja na mikopo ya asilimia 10 kwa ajili ya vijana ,wanawake na watu wenye ulemavu.
Fedha hii pia tumeipeleka Tarura zaidi ya sh. bilioni mbili kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu ya barabara jijini hapa,”amesema Iranqhe .
Meya huyo amesema kwa upande wa madarasa serikali iliwapatia sh.bilioni mbili kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 100 ikiwa lengo ni kuhakikisha wanafunzi wanaingia kwa pamoja na sio kwa awamu kama ilivyokuwa ikifanyika hapo awali.
Aidha amesema kuwa ujenzi wa madarasa unaendelea vizuri hadi sasa nakudai kuwa changamoto ya uboreshaji wa miundombinu hiyo kila mwaka unatokana na ongezeko la watoto wanaozaliwa.
Hata hivyo amesema kuwa ,lengo lao ni kuvuka lengo la asimilia 100 katika robo zote za mwaka huo hivyo anawasisitiza wananchi na wataalamu wa halmashauri hiyo kuendelea kutekeleza wajibu wao.
Pia Mstahiki Meya ameonya kundi la watu ambao wanatoa taarifa za uongo mtandaoni juu ya halmashauri hiyo kushuka kimapato ni vyema wananchi wakazipuuza taarifa hizo kwani sio za kweli na msemaji wa halmashauri hiyo ni Meya au Mkurugenzi na sio mwingine.