Na Josea Sinkala.
Ofisi ya mbunge wa jimbo la Momba Songwe Condester Michael Sichalwe imepanga kutumia shughuli ya michezo kuwaunganisha wananchi wake na fursa za kifedha kupitia wataalam wa uchumi wilayani Momba na kuibua na kuendeleza vipaji vya michezo na kuwafanya wananchi kuondokana na magonjwa yanayoepukika.
Akizungumzia maandalizi ya michezo hiyo mbunge huyo amesema aliahidi kwenye kampeni zake kuwa atahakikisha anaboresha sekta ya michezo jimboni kwake.
Condester (Mundi) amesema kupitia michezo mbalimbali itakayohusisha wananchi wa kata zake zote jimboni humo na kufanyika katika kijiji cha Chiwanda kata ya Nkangamo atawaalika wataalam wa uchumi kutoka taasisi za kifedha ili kutoa elimu ya mikopo na mambo mbalimbali kwa wananchi ili kujikwamua kiuchumi.
Amesema michezo hiyo itahusisha pia vijiji vyote 72 na vitongoji vingine kadhaa ili kufanya kufikia vijiji visivyopungua 100 ambapo elimu ya masuala ya fedha itatolewa kupitia vikundi mbalimbali ikiwemo madereva bodaboda.
Kwa mujibu wa mbunge huyo wa jimbo la Momba washindi watapata mamilion ya fedha na kombe kupitia Condester Cup hivyo wadau wa michezo na wananchi kwa ujumla wanaaswa kujitokeza kwenye michezo hiyo ambayo kilele chake kitafanyika Novemba 13 katika kijiji cha Mkulwe kata ya Nzoka na bonanza litakalofanyika katika kijiji na kata ya Ikana tarafa ya Ndalambo wilayani Momba Novemba 06, 2022.
Mbunge wa jimbo la Momba mkoani Songwe Condester Michael Sichalwe (Mundi) amekuwa na utaratibu wa kuandaa mabonanza ya michezo ili kuibua na kuendeleza vipaji vya michezo na kutumia mihadhara hiyo kutoa elimu ya masuala mbalimbali ya kimaendeleo na kueleza miradi mbalimbali ya kimaendeleo inayotekelezwa kwenye eneo lake (Momba)..