Muonekano wa sehemu ya barabara ya Malagarasi – Ilunde – Uvinza (km 51.1),
inayojengwa kwa kiwango cha lami, Mkoani Kigoma.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa (kulia) akimsikiliza Mhandisi
Mshauri wa Kampuni ya Norplan Mhandisi Henry Ngogoro (kushoto), hatua za ujenzi
wa barabara ya Malagarasi – Ilunde – Uvinza (km 51.1), inayojengwa kwa kiwango
cha lami, Mkoani Kigoma. Katikati ni Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara
Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Kigoma, Mhandisi Ngoko Mirumbe.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa (wa pili kulia), akimsikiliza
Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Tabora,
Mhandisi Raphael Mlimaji, hatua za ujenzi wa barabara ya Kazilambwa – Chagu
yenye urefu wa kilomita 36 inayojengwa kwa kiwango cha lami, Mkoani Tabora.
Muonekano wa hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa barabara ya Kazilambwa hadi Chagu
(km 36) inayojengwa kwa kiwango cha lami Mkoani Tabora. Ujenzi wa barabara hiyo
kwa sasa umefikia asilimia 65 na unatarajiwa kukamilika mwezi Januari, 20235
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa akiangalia uharibifu wa
miundombinu wa taa za barabarani katika Wilaya ya Urambo Mkoani Tabora. Kulia
ni Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Tabora,
Mhandisi Raphael Mlimaji.
Picha na WUU
…………………………….
Serikali imewaahidi wakazi wa Mkoa wa Tabora na Kigoma kuunganisha mikoa hiyo
kwa barabara za lami ifikapo mwakani 2023.
Akizungumza kwa nyakati tofauti mkoani Kigoma na Tabora wakati alipokagua miradi
iliyobakia kuunganishwa mikoa hiyo Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame
Mbarawa, amesema ujenzi wa barabara ya Malagarasi – Ilunde – Uvinza (km 51.1) na
Kazilambwa – Chagu (km 36) kwa kiwango cha lami ni azma ya Serikali ya kuunganisha
barabara zote za Mikoa na kuchochea shughuli za kibiashara katika mikoa hiyo na mikoa
jirani pamoja na nchi jirani za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Burundi.
“Serikali inayoongozwa na Mama Samia inaendeleza Sera ya Ujenzi kwa kuhakikisha
mikoa na wilaya zinaunganishwa kwa njia ya barabara bora sambamba na miradi mingine
ya uchukuzi ikiimarishwa ili kumpa uhuru mwananchi achague usafiri atakaouweza",
amefafanua Waziri Prof. Mbarawa.
Waziri Mbarawa amesema Serikali haitaongeza muda wa ziada kwa miradi hiyo miwili
na hivyo kumtaka Mkandarasi Kampuni ya STECOL Cooperation anayejenga barabara
hizo kukamilisha kwa wakati na viwango.
“Serikali haitaongeza muda wa ziada kwa miradi hii tunataka miradi hii iwe imekamilika
na wananchi wafaidi matunda ya kodi wanazolipa sababu fedha tayari mmeshalipwa
hivyo hakuna sababu nyingine za kuchelewesha kukamilika kwake", amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa.
Vilevile Waziri Prof. Mbarawa amekagua uharibifu uliofanywa kwenye miundombinu ya
taa za barabara katika Wilaya ya Urambo na kuomba uongozi wa Mkoa wa Tabora
kuchukua hatua stahiki kwa wananchi walioharibu miundombinu hiyo kwa kung’oa taa
saba na kuisababisha Serikali hasara ya takriban Shilingi Milioni 21.
Aidha, Waziri Prof. Mbarawa ametoa wito kwa wananchi kutofanya shughuli zozote
karibu na alama za mipaka ya barabara zilizowekwa kwani kufanya hivyo ni kosa
kisheria na hatua kali zitachukuliwa.
Kwa upande wake Meneja wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), Mkoa wa
Kigoma, Mhandisi Ngoko Mirumbe, amesema Wakala utahakikisha mkandarasi
anaongeza kasi ya ujenzi ili kutochelewesha kukamilika kwa mradi huo kwani unatakiwa
kukamilika Oktoba mwakani.
Naye Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), mkoa wa Tabora
Mhandisi Raphael Mlimaji, amemuhakikishia Waziri Mbarawa kuwa TANROADS itamsimamia Mkandarasi anayejenga barabara ya Kazilambwa hadi Chagu ili
kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati na viwango walivyokubaliana katika
mkataba.
Ujenzi wa barabara ya Malagarasi-Ilunde hadi Uvinza wenye kilomita 51.1 unaojengwa
kwa kiwango cha lami umefikia asilimia 17 na ujenzi wa barabara ya Kazilambwa hadi
Chagu yenye urefu wa kilomita 36 unaojengwa kwa kiwango cha lami umefikia asilimia
65.