Mkuu wa wilaya ya Iringa Mohamed Hassan Moyo akiongea kwenye mkutano wa hadhara wa kutatua mgogoro wa ardhi katika kijiji cha Mkumbwanyi
Kaimu Afisa Tarafa ya Pawaga Emmanuel Ngabuji akimuelezea mkuu wa wilaya historia ya mipaka ya kijiji cha Mkumbwanyi
Na Fredy Mgunda,Iringa.
Mkuu wa wilaya ya Iringa Mohamed
Hassan Moyo ameamuru kuondolewa kwa alama za mipaka ya Kijiji cha Mkumbwanyi,
Kisanga na Makuka iliyowekwa hivi karibuni baada ya kupokea malalamiko kuwa
alama hizo ziliwekwa kimakosa na kusababisha Migogoro ya baina ya vijiji hivyo
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara
katika Kijiji cha Mkumbwanyi, Mkuu wa wilaya ya Iringa alisema kuwa baada ya
kusikiliza malalamiko ya Wananchi wa Kijiji Cha Mkumbwani amejiridhisha kuwa
alama hizo za mipaka zimewekwa pasipo kushirikisha pande zote za Serikali za
vijiji jambo ambalo ni kinyume na taratibu.
Moyo amefafanua kuwa kwa mujibu wa
taratibu unapotaka kuweka alama za mipaka baina ya kijiji na Kijiji lazima
ushirikishe pale zote na ziridhie ni wapi Mpaka uwekwe ili kuepusha Migogoro
inayoweza kuhatarisha usalama wa Wananchi wa vijiji husika.
Awali kupitia taarifa iliyowasilishwa
katika Mkutano huo wa hadhara ilielezwa kuwa Maafisa wa Ardhi kutoka Wizarani
walifika Kijijini hapo Kwa lengo la kushughulikia mgogoro wa mipaka Lakini
kabla ya muafaka kamili waliweka alama hizo jambo lililotajwa kuwa batili na
lilolochochoa uhasama baina ya pande zinazopingana.
Licha kuamuriwa alama hizo kuondolewa
Kiongozi huyo wa Wilaya ya Iringa amemuagiza Kaimu Afisa Tarafa kupeleka
taarifa ya kusitishwa Kwa shughuli zote Katika maeneo yenye mgogoro wa
mipakahuku akiliamuru Jeshi la Polisi kumkamata yeyote atakayekwenda kinyume na
Amri hiyo
Alisema kwenye kushughulikia utatuzi
wa Mgogoro huo Serikali ya wilaya kupitia kamati ya Ulinzi na Usalama haitosita
kuchukua hatua Kwa Mtu yeyote wakiwemo viongozi wa vyama vya siasa kikiwemo
Chama Cha Mapinduzi watakajihusishakukaidi Amri hiyo wakati hatua za utatuzi
zikiendelea kufanywa na kamati hiyo
Afisa ardhi Mteule wa Halmashauri ya
Wilaya ya Iringa Geoffrey Kalua alisema kuwa kitendo cha Wataalam kutoka
Wizarani kuweka mipaka pasipo kushirikisha pande zote ni kinyume cha taratibu
hivyo maamuzi ya kuondoshwa kwa alama hizo yaliyotolewa na Mkuu wa Wilaya
Iringa Mohamedi Hassani Moyo ni maamuzi sahihi kisheria.
Kwa upande wake Kaimu Afisa Tarafa ya
Pawaga Emmanuel Ngabuji ameahidi kutekeleza agizo la kuondoa alama hizo
kwakushirikiana na Afisa Tarafa ya Isimani kama walivyoagizwa Huku Jeshi la
Polisi wilaya ya Iringa kupitia Mkuu wa Polisi wilaya akiahidi kuimarisha
Ulinzi wakati wa uondolewaji wa mawe ya alama za mipaka.
Awali akimueleza mkuu wa wilaya na
afisa ardhi Halmashauri ya wilaya ya Iringa, Diwani wa kata ya Mboliboli Yusuf
Msamba alisema kuwa toka zimewekwa alama hizo zimezua hali ya sintofahamu kwa
wananchi wa Kijiji cha Mkumbwanyi hivyo anauomba uongozi huo kutatua mgogoro
huo ili kurudisha amani iliyopotea kwa wananchi wote wa Kijiji hicho.
Msamba alisema kuwa maafisa ardhi
kutoka wizarani waliweka alama za mipaka ya Vijiji bila kushirikisha pande zote
mbili hivyo hilo lilikuja jambo ambalo ni kinyume cha sheria za ardhi na
zimesababisha kuibuka kwa mgogoro mpya ambao haukuwepi awali.