********************
Na Mwandishi wetu, Babati
WAANDISHI wa habari nchini wameaswa kuibua na kuandika habari na changamoto nyingi za jamii kuliko kuegemea na kuandika habari za viongozi wa Serikali pekee.
Rais wa Muungano wa klabu za waandishi wa habari nchini (UTPC) Deogratius Nsokolo ameyasema hayo mjini Babati kwenye mkutano mkuu wa klabu ya waandishi wa habari wa mkoa wa Manyara (MNRPC).
Nsokolo amesema waandishi wa habari nchini wana dhamana kubwa ya kuwasemea wananchi wasio na sauti hasa waliopo vijijini kwani hilo ni jukumu lao kubwa kuliko kuandika habari za viongozi pekee.
“Sisi ndiyo daraja la kuwafikisha wananchi wanyonge kwenye mamlaka husika ili changamoto zao za ukosefu wa maji, afya, shule na mengineyo zifike sehemu husika,” amesema Nsokolo.
Amesema wananchi wengi wanashindwa kufika kwenye mamlaka husika ikiwemo katika ofisi za wakuu wa wilaya au mikoa ila kupitia kalamu za waandishi wa habari changamoto zao sitaweza kusikika.
Mwenyekiti wa klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Manyara (MNPC) Zacharia Mtigandi ameeleza kuwa waandishi wa habari wa eneo hilo wamekuwa wakiandika changamoto nyingi za jamii.
“Waandishi wa Manyara wamekuwa wakiibua changamoto nyingi za jamii kupitia kalamu zao hivyo wanaendelea kutekeleza agizo lako la kujali kuandika habari za jamii kwa wingi,” amesema Mtigandi.
Hata hivyo, amesema klabu ya waandishi wa habari wa mkoa wa Manyara, wapo 18 na wameanzisha mfuko wao wa kujitegemea na hivi sasa una akiba ya sh500,000.