*****************
NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
CHUO Kikuu cha Dar es Salaam, Ndaki ya Uhandisi na Teknolojia Idara ya Uhandisi Mitambo na Viwanda imeandaa Kongamano la Kimataifa la Uhandisi wa Mitambo na Viwanda ili kutoa fursa kwa watafiti kujadiliana na watafiti wengine kuhusu matokeo ya tafiti na bunifu zao katika kufanikisha ufanisi na tija ya sekta ya viwanda.
Kongamno hilo litafanyika katika ukumbi wa Maktaba mpya ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuanzia Oktoba 20 hadi 21, 2022 huku kauli mbiu ya Kongamano hilo la 7 la Kimataifa na maonesho ya Uhandisi wa Mitambo na Viwanda ni “Kukuza Uendelevu wa Viwanda vinavyotegemea Maliasili katika Uzalishaji kupitia Sayansi, teknolojia na Ubunifu”.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 19,2022 Jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Idara ya Uhandisi Mitambo na Viwanda Dkt.Innocent Macha amesema wajumbe wapatao 200 kutoka Tanzania na nje ya nchi wanatarajia kushiriki Kongamano hilo.
Amesema Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Prof.Adolf Mkenda anatarajiwa kuzindua Mkutano huo Oktoba 20,2022 huku majadiliano yatafanyika katika maeneo makuu matatu ya malighafi na uzalishaji, Nishati na Usimamizi wa Viwandana pia kutakuwepo maonesho ya tafiti na bunifu kutoka kwa wadau mbalimbali.
“Malengo mengine ya mkutano huu ni kuimarisha uhusiano kati ya idara na wadau wengine hususani viwanda. Hii ni kwasababu tunathamini sana mchango wa viwanda na waajiri wa wahitimu wetu katika kuboresha taaluma na huduma zetu”. Amesema