Serikali ya Tanzania na Poland zimekubaliana kuendelea kuimarisha ushirikiano
kwenye sekta mbalimbali zenye manufaa kwa nchi hizi mbili ikiwemo kilimo,
elimu, nishati, utalii,
biashara na uwekezaji.
Makubaliano hayo yamefikiwa leo tarehe 18 Oktoba 2022 jijini Warsaw,
Poland wakati wa mazungumzo rasmi yaliyofanyika kati ya Waziri wa Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax na Waziri
wa Mambo ya Nje wa Poland, Mhe. Zbigniew Rau.
Wakizungumza na waandishi wa habari mara baada ya mazungumzo hayo,
Mawaziri hao wamesema Tanzania na Poland
ambazo zinaadhimisha miaka 60 ya ushirikiano, zina fursa nyingi zenye manufaa
kwa pande zote mbili na kwamba wamekubaliana kuweka mikakati madhubuti ya
utekelezaji wa makubaliano hayo ikiwa ni pamoja na kuanzisha ushirikiano kwenye
maeneo mapya ya ulinzi na usalama pamoja na nishati.
Akizungumza, Mhe. Dkt. Tax amesema Poland
imeandelea kuwa mshirika muhimu wa kimkakati kwa Tanzania katika kipindi chote
cha miaka 60 ya ushirikiano wa kidiplomasia, na kwamba wamekubaliana kuendelea
kushirikiana kwenye sekta ambazo zimekuwa na tija kubwa kwenye ushirikiano huo
ikiwemo kilimo, elimu, utalii, biashara na uwekezaji.
“Katika majadiliano yetu leo, tumetathmini
ushirikiano wetu katika maeneo ambayo tayari tunashirikina na Poland kama
kilimo, elimu, biashara na uwekezaji na utalii. Pia tumekubaliana kuongeza
maeneo ya ushirikiano katika masuala ya
nishati na ulinzi na usalama ambayo ni muhimu katika kukuza ushirikiano wetu”
amesema Dkt. Tax.
Kadhalika Mhe. Dkt. Tax ametumia fursa hiyo
kuwakaribisha wawekezaji na wafanyabiashara kuja nchini kuwekeza kwani Tanzania
bado inazo fursa nyingi za uwekezaji. Aidha, Mhe. Dkt. Tax
ameipongeza Serikali ya Poland na Wananchi wake kwa kuendelea kuichagua
Tanzania kama kituo chao muhimu cha utalii ambapo nchi hiyo ni miongoni mwa
nchi tano za juu zenye idadi kubwa ya watalii waliotembelea nchini mwaka
2022.
“Ni imani yangu kuwa, baada ya ziara yangu
hii biashara, uwekezaji, utalii na ushirikiano wa kisiasa kati ya Tanzania na
Poland utaimarika zaidi. Pia kipekee nitumie fursa hii kuwashukuru wananchi wa
Poland kwa upendo wao kwa Tanzania. Kwani kwa mwaka huu 2022, Poland ni
miongoni mwa nchi tano zilizoshika nafasi ya juu kwa wananchi wake kutembelea
nchini kwetu nawashukuru sana na karibuni tena, alisisitiza Dkt. Tax.
Kwa
upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Poland, Mhe. Zbigniew Rau amesema kuwa
nchi yake inathamini ushirikiano wa kihistoria uliopo kati yake na Tanzania na kwamba
maeneo muhimu yaliyojadiliwa na kukubaliwa wakati wa mkutano wao yatatekelezwa
na Serikali ya nchi hiyo.
“Tanzania ni mshirika muhimu sana kwa
Poland na miongoni mwa nchi zinazopewa kipaumbele katika program za muda
mrefu za maendeleo ikiwemo uwekezaji kwenye sekta ya kilimo,” amesema Mhe. Rau.
Pia alitumia fursa hiyo kumshukuru Mhe.
Dkt. Tax kwa kukubali mwaliko wake na kuitembelea Poland ambapo alisema hatua
hiyo ni muhimu katika kukuza ushirikiano kati ya nchi mbili kwani utaharakisha
utekelezaji wa makubalino mbalimbali ambayo tayari yapo na mapya.
“Tumekuwa na mazungumzo yenye tija na Mhe.
Waziri Dkt. Tax. Kupitia mazungumzo hayo ushirikiano wetu utaimarika zaidi. Nitumie
fursa hii kumshukuru Mhe. Waziri na ujumbe wake kwa kukubali mwaliko wangu na
kututembelea”, amesema Mhe. Rau.
Wakati huohuo, Mhe. Dkt. Tax ametembelea na kuweka shada la
maua kwenye kaburi la askari mashujaa wa nchi hiyo lililopo jijini Warsaw.
Mhe.
Dkt. Tax yupo nchini Poland kwa ziara ya kikazi ya siku tatu kuanzia tarehe 17
hadi 19 Oktoba, 2022, ambayo pamoja na mambo mengine inalenga kuimarisha
ushirikiano wa kidiplomasia na kiuchumi baina ya nchi hizi mbili.
Katika
ziara hiyo Mhe. Waziri Tax amefuatana na Wajumbe kutoka Wizara ya Ulinzi na
Jeshi la Kujenga Taifa. Wizara ya Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kituo cha Uwekezaji Tanzania
(TIC), Mamlaka ya Ukuzaji Biashara na Uwekezaji Zanzibar (ZIPA), Wakala
wa Taifa wa Hifadi ya Chakula (NFRA), Benki Kuu ya Tanzania (BOT) na Shirika la
Maendeleo la Taifa (NDC).
Sehemu ya ujumbe wa Tanzania ulioshiriki mazungumzo kati ya Mhe. Dkt. Tax na Mhe. Rau. Kulia ni balozi wa Tanzania nchini Ujerumani na Poalnd, Mhe. Abdallah Possi |
Sehemu ya ujumbe wa Poland wakati wa mazungumzo hayo |
Mhe. Waziri Dkt. Tax na mwenyeji wake, Mhe. Rau wakizungumza na waandishi wa habari kuhusu masuala mbali mbali ya ushirikiano waliyojadili na kukubaliana |
Sehemu ya Ujumbe wa Tanzania akiwemo Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikisno wa Afrika Mashariki, Balozi Swahiba Mndeme (Kushoto) |
Mhe. Waziri akisindikizwa na Naibu Mkuu wa Itifaki wa Poland, Bw. Artur Harazim kwenye kaburi la askari mashujaa wa Poland kwa ajili ya kuweka shada la maua kwa lengo la kuwaenzi na kuwakumbuka |
Gwaride la heshima liloandaliwa rasmi kwa ajili ya Mhe. Dkt. Tax alipofika eneo hilo kwa ajili kuwakumbuka mashujaa wa Poland |
Mhe. Dkt. Tax akisaini kitabu cha wageni alipowasili kwenye eneo hilo la makumbusho ya mashujaa |
Mhe. Waziri Dkt. Tax akiwa na ujumbe wa Tanzania na Poland mara baada ya kukamilisha shughuli ya uwekaji shada la maua kuwakumbuka askari mashujaa wa Poland |