Na Victor Masangu,Kibaha
WANANCHI wa Kijiji cha Kimara Misale kata ya Dutumi Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani wameondokana na kero ya siku nyingi ya ukosefu wa
ya maji Safi na salama waliyokuwa nayo kwa muda mrefu baada ya kukamilika kwa mradi wa maji uliotekelezwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA).
Wakazi hao kwa muda mrefu walikuwa wakitumia maji ya mto Ngerengere na Ruvu jambo ambalo wanaeleza kuwa lilikua kero kwao kutokana na baadhi yao kuliwa na mamba na wengine kupata ulemavu waliosababishiwa na mamba katika mto Ruvu.
Wakizungumza muda mfupi baada ya kukabidhiwa mradi wa maji na RUWASA walisema awali walikuwa wakitembea umbali wa kilometa mbili hadi tano kufuata huduma hiyo.
Nasra Jafari ameshukuru Serikali kwa hatua hiyo ambayo inawezesha sasa kufanya kazi zao za nyumbani kwa wakati tofauti na zamani ambapo walikua wanachelewa kutekeleza majukumu yao kwa kukosa maji.
Naye Diha Kunga (70) amesema kitendo cha Serikali kuwafikishia maji katika kijiji chao kimewasaidia wazee ambao kwasasa wanapata maji karibu na wanapoishi bila malipo tofauti na awali ambapo walilazimika kutumia muda mwingi kwenda mtoni na kuomba msaada kwa ndugu.
“Hawa RUWASA wametufanyia jambo kubwa tangu kijiji hiki kuanzishwa mwaka huu ndio tunapatiwa maji tena sisi wazee tumepata msamaha kila siku tunachota bure hili ni jambo la faraja kwetu” amesema Diha.
Akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya mradi huo Meneja wa RUWASA Mhandisi Debora Kanyika amesema mradi huo umetekelezwa na Mkandarasi kampuni ya Buildall Constractors kwa gharama ya sh. 498,709,539.89 fedha za UVIKO-19 na kwamba wananchi 1,700 watanufaika.
Mhandisi Kanyika amesema mradi huo umehusisha ujenzi wa tanki la juu la lita 50,000 kwenye mnara wa mita 12, vituo nane vyenye vichotea maji viwili viwili, uchimbaji wa visima viwili katika vitongoji vya Kimara na Kigogo, nyumba ya mashine, ufungaji wa umeme wa jua na uchimbaji ulazaji wa mabomba na ufukiaji wa mtandao wa maji upatao kilomita 8.4.
Meneja huyo amesema kwasasa mradi huo umefikia asilimia 98 ambapo wananchi wanapata maji kwa usimamizi wa Jumuiya ya Watumia maji kijiji cha Kimara Misale wakati mkandarasi akiwa katika hatua za mwisho.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Kimara Misale Salum Mtego amesema upatikanaji wa mradi huo unawaondoa wananchi kwenye adha ya kutembea umbali mrefu na kuchota maji mto Ruvu.
Mtego amesema sasa wananchi wataondokana na adha ya kuliwa na mamba kwani wapo watu wanne ndani ya miaka zaidi ya miwili wameliwa na mamba wakiwa wanachota maji kwenye mto Ruvu.
Naye Mwenyekiti wa bodi ya Maji kimara Misale Sudi Omari amesema wametoa msamaha kwa wazee zaidi ya 40 kupata maji bure ndoo nne kila siku pamoja na walemavu wawili huku wananchi wengine wakipata huduma hiyo kwa sh 100 kwa ndoo tatu.