************************
Madereva wanaondesha vyombo vya moto wametakiwa kusoma tabia za Wanafunzi wanapovuka barabara ili kuepusha ajali zisizikuwa na msingi kwa wanafunzi na kukatisha ndoto zao na malengo kwa kuwasababishia vifo na ulemavu wa kudumu.
Wito huo umetolewa leo Jumatano Oktoba 19 Jijini Dar es salaam na mkaguzi msaidizi wa polisi Dumu Mwalugenge kutoka kikosi cha usalama barabarani makao makuu kitengo cha elimu wakati wa zoezi la utoaji wa elimu ya usalama barabarani katika shule ya Msingi Msasani B Wilaya ya Kinondoni lililoratibiwa na taasisi ya Tanzania Road Safety Initiative kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kikosi cha usalama barabarani.
Mwalugenge amesema kuwa wanafunzi wamekuwa na tabia ya kuchomoka na kukimbia ghafla wakati wakivuka barabara na kupelekea kugongwa na gari au pikipiki hivyo ni muhimu kwa madereva wakajua tabia za watoto na kupunguza mwendokasi wanapopita kwenye maeneo ya shule ili kuepusha ajali.
“Tunaelewa namna ambavyo watoto wa shule wamekua wakiathirika na ajali za barabarani haswa wanapokua wanatoka majumbani kuja shuleni au kutoka shuleni kwenda nyumbani hivyo sisi kama jeshi la Polisi tumeweka nguvu zetu kwenye elimu kwa watoto ili kuwajengea uwezo wa kuweza kuepuka ajali” amesema
Ameongeza kuwa elimu hiyo waliopatiwa watoto hao itawajengea uwezo wa kutumia barabara kwa usalama na kufahamu sheria za usalama barabarani zitakazowasaidia kujiepusha na ajali .
Kwa upande wake Katibu wa taasisi ya Tanzania Road Safety Initiative Bw. Hashim Rajab Kifaru amesema utoaji wa elimu ya usalama barabarani kwa wanafunzi ni mpango kazi wa utoaji wa elimu hiyo katika Manispaa ya Kinondoni kwa lengo la kuwajenga vijana waweze kufahamu kanuni na sheria za barabara ili kuepukana na ajali zinazoweza kuepukika.
Baadhi ya wanafunzi waliopatiwa elimu ya usalama barabarani wameeleza kuwa watatumia elimu hiyo vizuri pindi wanapovuka barabara na watakua mabalozi wazuri kwa wenzao ambao hawakubahatika kupata elimu hiyo kuwaelekeza walochofundisha ili kuepuka ajali.