Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na watumishi wa umma wa wilaya ya Namtumbo kwenye makazi ya Mkuu wa Wilaya hiyo Mkoani Ruvuma, Oktoba 18, 2022. Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma , Kanali Thomas Laban. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
***********************
- Aagiza milango zaidi ya 10 ing’olewe, akuta varnish imepakwa leo
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekagua ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Namtumbo na kusema Serikali haiwezi kukaa kimya huku baadhi ya watumishi wakifanya vitendo vya hovyo.
“Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ameleta shilingi bilioni 7 za ujenzi wa hospitali hii. Fedha hizi za ujenzi ni lazima wananchi waone thamani ya fedha zao. Siwezi kukubaliana na utendaji wa hovyo. Fedha ziko hapa tangu Aprili, ni kwa nini hadi sasa majengo yapo kwenye lenta? Huu ni ubabaishaji,” amesema.
Waziri Mkuu ametoa onyo hilo leo (Jumanne, Oktoba 18, 2022) wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Migelegele mara baada ya kukagua ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Namtumbo, mkoani Ruvuma.
“Nimekagua ujenzi wa hospitali ya wilaya lakini sijaridhishwa na hali ya ujenzi. Nimeagiza milango yenye hitilafu yote ing’olewe na iwekwe yenye hadhi ya hospitali ya wilaya. Iweje imeacha nafasi juu hadi vidole vinapita? Mtu akifunga mlango wewe uliyeko nje unaona ndani. Hii haikubaliki, RC simamieni milango hiyo itolewe, na ije yenye hadhi,” amesisitiza.
Mapema akikagua ujenzi wa hospitali hiyo, Waziri Mkuu alikuta baadhi ya milango imepishana urefu licha ya kuwa inapaswa ikutane ili kitasa kiweze kufunga. Mingine ilikuwa inagoma kufunga, inarudi nyuma na kubakia wazi. Pia aligusa mlango na kukuta varnish bado haijauka.
Akizungumzia kuhusu upatikanaji wa mbolea, Waziri Mkuu amesema Rais Samia alitoa ruzuku ya sh.bilioni 150 ili kushusha bei ya mfuko wa mbolea na kuwaeleza wakazi hao kwamba mkoa huo umepangiwa makampuni matano ya kusambaza mbolea.
“Makampuni matano ya Mohammed Enterprises, Yara, OCIP, Premium na ETG yamepangiwa kuleta mbolea hapa mkoani, na hadi sasa tayari tani za mbolea 9,000 zimeshawasili. Kati ya hizo, tani 2,467 zimeshaenda vijijini.”
“Mahitaji ya mkoa mzima ni tani 67,000 kwa hiyo hizi tani 9,000 hazitoshi. Watu wa TFL simamieni ili iletwe haraka. Mbolea za kupandia zije sasa na za kukuzia zije baadaye. Jitahidini kuongeza idadi ya mawakala ili wananchi wafikiwe huko waliko,” amesisitiza.
Mapema, akizungumza na wananchi hao, Waziri wa Nchi (OR-UTUMISHI), Bibi Jenista Mhagama aliishukuru Serikali ya Rais Samia kwa ujenzi wa hospitali na kwamba wanufaika wakubwa ni wanawake, watoto na wazee.
Alisema Serikali itaendelea kuwapangia watumishi wa sekta ya afya ili waweze kufika kutoa huduma kwenye hospitali hiyo. “Mwaka 2022/2023 Serikali itaajiri watumishi 30,000 kwenye ajira mpya, na wengi ni wa sekta ya afya na elimu,” alisema.
Naye, Naibu Waziri wa Nchi (OR-TAMISEMI), Bw. David Silinde alisema Rais Samia ameamu kujenga shule za wasichana katika mikoa yote 26 na iliyopo katika Halmashauri ya Namtumbo ni miongoni wa shule 10 za kwanza nchini ambazo zimepatiwa fedha mwaka huu.
“Shule hizi zimetengewa shilingi bilioni 4 kila moja na zikikamilika zitakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi kati ya 1,000 na 1,200 ambao watakuwa wanasoma masomo ya sayansi.”
Naye, Mbunge wa Namtumbo, Bw. Vita Kawawa alisema anamshukuru Rais Samia kwa kutoa sh. bilioni 15.5 kwa ajili ya shughuli za maendeleo wilayani humo. Pia aliishukuru Serikali kwa kuwapatia mradi ya maji wa sh. bilioni 5 ambao umesaidia wananchi kupata maji bila mgao.