Mkuu wa mkoa wa Arusha,John Mongela akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maonyesho hayo yatakayofanyika jijini Arusha kesho.
*****************************
Julieth Laizer,Arusha
Arusha. Naibu waziri wa uwekezaji, viwanda na biashara Exaud Kigahe anatarajiwa kufungua maonyesho makubwa ya siku saba ya viwanda vidogo vidogo (SIDO)Kanda ya kaskazini yanayotarajia kufanyika katika viwanja vya makumbusho Jijini Arusha.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo Octoba 18, Mkuu wa mkoa wa Arusha John Mongela amesema kuwa maonyesho hayo yataanza kesho Octoba 19 na kufikia tamati Octoba 25 mwaka huu.
“Maonyesho haya yatashirikisha zaidi ya wajasiriamali 200 kutoka kanda ya kaskazini, watakaoonesha bidhaa mbali mbali wanazotengeneza na zilizoongezwa thamani ikiwemo bidhaa za uhandisi , vyakula vya usindikaji, kazi za mikono zilizotengenezwa Kwa ngozi, nguo na bidhaa mchanganyiko zenye matumizi tofauti”
Amesema kuwa mbali na wajasiriamali hao pia wamewalika wawekezaji kutoka sekta za mnyororo mzima wa viwanja na biashara, wagavi, wahusika wa malighafi za viwandani pia waajiiri ili kuwapa vijana wenye uwezo wa kubuni na kutengeneza bidhaa mbali mbali fursa za kupata pesa kupitia shughuli zao.
“Katika maonyesho haya pia ziko taasisi za kifedha zinazojihusisha na maendeleo ya viwanda ili kutoa elimu ya fursa mbali mbali walizonazo kwa vikundi vya vijana na wajasiriamali hasa mikopo ya bei nafuu kwa wale waliojiajiri na zaidi watakuwepo wataalamu, washauri na wadau wengine wa maendeleo ya viwanda kutoa elimu” amesema Mongela .
“Wakati mwingine wanaweza kuwa tiyari kuanzisha shughuli za uzalishaji mali lakini ukakosa muongozo na ujuzi pia ukapata vyote lakini mtaji ukawa tatizo, ndio maana tumekuja na maonyesho haya ili kutatua matatizo hayo lengo letu ni kuisaidia kupunguza wimbi la vijana wasio na ajira wala shughuli ya kipato waje kuchangamkia fursa”ameongeza Mongela.
Nae Meneja wa SIDO mkoa wa Arusha, Jalphary Donge amesema kuwa maonyesho hayo ni ya 17 kufanyika nchini tangu kuanzishwa ambapo mwaka huu yana kauli mbiu ‘pamoja tujenge viwanda kwa uchumi na ajira endelevu’.
Donge amesema lengo ni kuwakutanisha wajasiriamali kwa ajili ya kuhamasisha ubora wa bidhaa wanazotengeneza, kukuza soko la wajasiriamali Kanda ya kaskazini lakini pia kuhamasisha watu waweze kupenda bidhaa za ndani baada ya kuja kuona ubora uliyopo.
“Maonyesho haya yaliyoanzishwa SIDO ni mpango wa kuwasaidia vijana kukabiliana na tatizo la ajira na ukuzaji wa uchumi nchini ambao utaenda sambamba na kuwasaidia kuwakutanisha na taasisi, makampuni na mashirika binafsi yanayohudumia wajasiriamali ikiwemo mikopo, bima, uthibiti ‘TBS’ na masoko”ameongeza.