Kaimu mkuu wa chuo cha ufundi Arusha,Dk Musa Chacha akizungumza katika semina hiyo jijini Arusha.
Mkurugenzi msaidizi wa usalama mtandao kutoka wizara ya habari ,mawasiliano na teknolojia ya habari, Mhandisi Stephen Wangwe akizungumza katika semina hiyo jijini Arusha leo.
Mtaalamu wa usalama mtandao na uchunguzi wa makosa ya kidigitali ,Yusuph Kileo akizungumza katika semina hiyo jijini Arusha.
*****************
Julieth Laizer,Arusha.
Serikali kupitia mkakati wa Taifa wa utoaji wa elimu kwa umma imeanza kufikia makundi mbalimbali ikiwemo watu wenye ulemavu juu ya usalama wa mitandao kwa lengo la kujiepusha na vitendo vya kihalifu.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Msaidizi wa usalama wa mtandao kutoka Wizara ya Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari,Mhandisi Stephen Wangwe,wakati akitoa elimu hiyo katika taasisi mbalimbali jijini Arusha kama maadhimisho ya watumiaji wa usalama wa mtandao kupitia makubaliano ya Dunia kuwa kila ifakapo Mwezi Oktoba.
Mkurugenzi huyo amesema kutokana na kukithiri kwa vitendo vya kihalifu mitandaoni hali inayopelekea uzalilishaji,unyang’anyi wa akauti(kudukua) imepelekea kupitia mkakati wa mwaka 2018 katika utoaji wa elimu kwa umma katika makundi hayo.
“Serikali inamkakati wa Taifa wa usalama wa mtandao wa tangu mwaka 2018 ambao kazi yake inaangalia wadau wote katika tasnia na mamlaka mbalimbali ikiwa kila mmoja anapatiwa jukumu lake katika utekelezaji ili kuwa na utaratibu mzuri wa kushirikiana,”amesema Mkurugenzi huyo.
Pia amesema wanao mkakati wa utoaji wa elimu kwa umma kwani katika mamlaka hizo wanaweza kuwa na mifumo mizuri lakini pasipokuwa na elimu kwa wananchi kutaongeza mianya mingi ya uhalifu wa mitandaoni.
Kwa upande wake Mtaalamu wa usalama mtandao na uchunguzi wa makosa ya kidijitali ,Yusuph Kileo ameshauri watumiaji wa mitandao kuzingatia kujilinda wenyewe kwa kuhakikisha wanatumia nywila katika simu zao ili kuepuka uhalifu.
“Vilevile tumekuwa tukiwahamasisha wati kuwa makini wanapofanya shughuli mbalimbali mitandaoni mfano katika kuangalia taarifa wanazoweka mitandaoni ili isijekuwa chanzo cha wao kuwa katika uhalifu,”amesema Mtaalamu huyo.
Pia amesema wamekuwa wakihamasisha watu kuwa na tabia ya kuripoti matukio ya kihalifu ya mitandaoni pindi wanapokutwa hali hiyo imetokana na uwepo wa changamoto ya baadhi ya watu kukaa kimya hali inayopelekea wahalifu kuendelea kudhuru wengine,”alisema Kileo Mtaalamu wa Usalama Mtandao.
Kileo ameongeza kuwa,katika kipindi hiki uelewa wa usalama wa mitandao umekuwa kwa kiasi kikubwa tofauti na hapo awali walikuwa wanapata changamoto kubwa kutokana na watu kuwa na uelewa mdogo juu ya usalama wa mitandao yao.
“Pia elimu hii ambayo inakuja kupitia mkakati wa kitaifa nina imani itawafungua watu wengi zaidi na sisi katika umoja wa wanausalama wa mtandao wa nchi za Afrika tulikubaliana kuwa lazima elimu ya uelewa lazima watu wapate,”amesema.
Naye Kaimu Mkuu wa chuo cha Ufundi Arusha,Dkt.Musa Chacha amesema mafunzo hayo ni muhimu katika hutoaji wa huduma katika Taasisi hiyo ikiwemo ulipaji wa ada,Makusanyo mbalimbali hivyo chachu kwao katika kujihimarisha katika kuhakikisha watu wanaofanya wizi mitandaoni wasifanikiwe adhma yao.
“Tunatamani mafunzo haya yakaendelea kuwepo ili chuo hicho waweze kujiandaa katika kuwaalika wizara ya habari,mawasiliano,Teknolojia na Habari ili watufundishe zaidi na familia zetu pamoja na wanafunzi wote kwa lengo la kufahamu na kuweka ulinzi wa mtandao yetu,”amesema Dkt.Chacha.