Matukio mbali mbali za washiriki katika mafunzo hayo ambayo yamefanyika katika Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani.
************************
Na Victor Masangu,Bagamoyo
Katika kukabiliana na changamoto iliyopo kwa baadhi ya watoto kusahaulika kupata fursa ya elimu ya awali Ofisi ya elimu Mkoa wa Pwani kupitia mradi wa shule bora imeamua kutoa mafunzo ya siku tano kwa wasaidizi jamii wa walimu (MJM) lengo ikiwa ni kuwaandaa kwenda kuwafundisha watoto wadogo katika vituo vya utayari 36 vilivyoanzishwa.
Hayo yamebainishwa na Afisa elimu vifaa na takwimu katika halmashauri ya Chalinze Harord Chungu ambayo pia alikuwa mwezeshaji katika mafunzo hayo ya kuwajengea uwezo na mbinu ya kufundisha ambayo yamefanyika katika shule ya Sekondari Bagamoyo na kuhudhuliwa na maafisa elimu mbali mbali.
Aidha alisema kwamba mafunzo hayo yameweza kuwashirikisha wasaidizi jamii wa mwalimu kutoka katika halmashauri zote za Mkoa wa Pwani na kwamba wataweza kujifunza mambo mbali mbali yanayohusiana na jinsi ya kuwafundisha watoto hao wadogo.
“Hawa washiriki wanapatiwa mafunzo ya jinsi ya kuwajengea uwezo zaidi namna ya kuwafundisha watoto hao wadogo ambao watakuwa katika vituo vya utayari kwa kutumia mbinu mbali mbali ikiwemo kwa njia ya vitabu na njia nyinginezo,”alisema
Kwa upande wake Afisa elimu ya watu wazima Wilaya ya Kisarawe Ester Senkoro alisema kuwa mafunzo hayo yamelenga zaidi kwenda kuimarisha watoto hao kupata elimu kabla ya kujiunga na darasa la kwanza msimu wa mwaka 2023.
Nao baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo ya MJM akiwemo Joyce Thobias na Abdulkadilia wamesema kwamba kupitia mpango huo wa shule bora utaweza kuwapa fursa ya kwenda kuyafanyia kazi ya ufundishaji katika vituo hivyo vya utayari kwa lengo la kuboresha elimu kuanzia ngazi ya awali.
Afisa Elimu Wilaya ya Bagamoyo Wema Kajigili pamoja na Mkuu wa Shule ya Bagamoyo Sekondari Ombeni Ally wamesema kwamba mafunzo hayo ni umuhimu Sana na yataweza kuleta tija zaidi ya kuwasaidia watoto wadogo.
Mafunzo hayo ya siku tano yameandaliwa na Ofisi ya elimu Mkoa wa Pwani kwa ufadhili wa uingereza Ukaid kupitia mradi wa shule bora nchini ili kuwawezesha watoto kupata elimu ya awali kabla ya kujiunga na darasa la kwanza mwaka 2023.
Mradi huo wa shule bora unatekelezwa katika mikoa tisa ambayo ni Simiyu,Tanga,Dodoma,Pwani,Mara,Katavi,Kigoma,Singida,pamoja na Mkoa wa Rukwa.