Na John Walter-Babati
Mwili wa Mohamedi Musa Said (42) anaedaiwa kuuawa na kikosi cha ulinzi shirikishi (Sungusungu) wa usiku mjini Babati katika mkoa wa Manyara, umezikwa oktoba 17,2022 nyumbani kwao mtaa wa Kwere mjini hapa.
Baba mlezi wa familia ya Mohamedi anasema Sungusungu hao walimpiga na kumpa mateso makali mtoto wao kwa kumchoma moto kwa kutumia nailoni kisha kumtelekeza mashambani ambapo alikosa msaada wa haraka na kupelekea kifo chake.
Baadhi ya wakazi mjini Babati wameiomba serikali kuingilia kati suala hilo kwa kuwa tukio hilo sio la kwanza kufanywa na sungusungu kwani walishamfanyia ukatili huo wa vipigo na kumchoma moto mwananchi mwingine na kumuachia majeraha katika mwili wake.
Wengine wameeleza kuwa vikundi hivyo baadhi yao sio waaminifu wamekuwa wakijihusisha na uporaji na wizi wa mali za watu.
Kaimu kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Manyara Kamishna msaidizi wa Polisi Yahaya Athumani amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba watuhumiwa sita wanashikiliwa kwa tuhuma za mauaji hayo kwa hatua zaidi za kisheria.
Kaimu kamanda amesema Oktoba 14 usiku mtaa wa Nyunguu mjini Babati, Sungusungu wakiwa katika doria walimkamata Mohamedi ambaye ni marehemu kwa madai ya wizi ambapo walienda nae hadi nyumbani kwake mtaa wa Kwere lakini hawakukuta chochote walichodai kuwa kimeibwa na kisha kumpiga bila kumfikisha kituo cha polisi wala hospitali.
Aidha kamanda Athumani ametoa wito kwa vikundi vya ulinzi shirikishi kuacha kujichukulia sheria mkononi na badala yake wanapomkamata mtuhumiwa wamfikishe katika kituo cha polisi.