**************************
Na John Walter-Manyara
Mkuu wa mkoa wa Manyara Charles Makongoro Nyerere amesema mkoa huo umepata heshima kubwa kwa kufanyika maonesho maadhimisho makubwa ya fimbo nyeupe ambayo yanatarajiwa kufanyika katika uwanja wa Kwaraa mjini Babati kuanzia Oktoba 19-23, 2022.
Mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho hayo anatarajiwa kuwa waziri mkuu Kassim Majaliwa.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa wakati akitoa taarifa kuhusu maadhimisho hayo, Nyerere amesema yatatanguliwa na Kongamano la siku mbili kwa Watu wasio ona litakalofanyika katika ukumbi wa chuo kikuu huria Manyara Oktoba 18 na 19 kujadili masuala mbalimbali na changamoto zinazowakabili watu wasio ona.
Amesema Mkoa wa Manyara umepata fursa hiyo na itaweza kutangaza fursa mbalimbali zinazopatikana ikiwemo Utalii, madini na ufugaji kwa wageni zaidi ya 1,000 watakaohudhuria kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania.
Pia mkuu wa mkoa amesema maadhimisho hayo yataenda sambamba na maeonesho ya biashara ambapo itakuwa ni fursa kwa wafanyabiashara na wajasiriamali kunoesha bidhaa zao.
Kwa Mujibu wa Katibu wa TCCIA mkoa wa Manyara Mwanahamisi Hussein maandalizi ya maonesho ya biashara yamekamilika ambapo kwa sasa makampuni, mashirika na taasisi zinaendelea kuweka bidhaa zao katika mabanda yaliyoandaliwa.
Naye katibu tawala mkoa wa Manyara Carolina Mthapula amewataka wakazi wa mji wa Babati kuwa wakarimu kwa wageni na boda boda kuwa waaminifu kwa wateja watakaowabeba.
Mwenyekiti wa chama cha Wasio ona nchini (TLB) Omari Sultan Mpondelwa akielezea maadhimisho hayo amesema, ni siku maalumu ambayo huadhimishwa kote ulimwenguni kwa ajili ya watu wenye ulemavu wa macho (hasa wale waliopoteza uoni, yaani wasioona).
Ameeleza kuwa Fimbo nyeupe, ni fimbo maalumu inayotumika na mtu asiyeona, ili kumtambulisha kwa watumiaji wengine wa barabara , wakati wowote na hasa anapokuwa akitembea ikiwa ni matokeo ya athari ya vita vya pili ya Dunia.