Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwapungia wananchi wakati alipokagua maendeleo ya ujenzi wa Stendi Kuu ya Mabasi Nyegezi jijini Mwanza akiwa katika ziara ya siku tatu Mkoani humo,
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa mhandisi wa mradi wa ujenzi wa Stendi Kuu ya Mabasi Nyegezi jijini Mwanza, Mhandisi Henry Joseph (kushoto ) wakati alipokagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo jijini, Oktoba 17, 2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
……………………….
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Watanzania wajipange kikamilifu kutumia fursa zitokanazo na miradi mbalimbali ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan.
Ameyasema hayo leo (Jumatatu, Oktoba 17, 2022) baada ya kukagua miradi ya ujenzi wa Stendi Kuu ya Mabasi Nyegezi pamoja na ujenzi wa Meli ya MV Mwanza Hapa Kazi Tu akiwa katika ziara ya kikazi ya siku tatu ya kukagua miradi ya kimkakati inayotekelezwa mkoani Mwanza.
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwahakikishia wananchi kuwa hakuna mradi wowote wa kimkakati utakaokwama kwani Serikali imejipanga kikamilifu kwa kutenga fedha za kutosha kwa ajili ya kuikamilisha. “Endeleeni kuiamini Serikali yenu.”
Ujenzi wa mradi wa Stendi Kuu ya Mabasi Nyegezi unatarajiwa kugharimu zaidi ya shilingi bilioni 15 na utakapokamilika mwishoni mwa mwaka huu utachukua mabasi makubwa 120 na magari[m1] madogo 80, pia unategemea kuiingizia Halmashauri ya Jiji la Mwanza shilingi bilioni 2.5 kwa mwaka. Kwa sasa mradi huo umefikia asilimia 98.
Akizungumzia kuhusu mradi wa ujenzi wa meli ya MV Mwanza Hapa Kazi Tu, Mheshimiwa Majaliwa amesema kwa sasa ameridhishwa na kazi inayoendelea na kwamba ameendelea kumsisitiza mkandarasi ahakikishe mradi huo unakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyohitajika. “Nimefurahi kuona meli imefikia hatua hii.”
Mei 7, 2022 Mheshimiwa Majaliwa alifanya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa Meli ya MV Mwanza Hapa Kazi Tu na aliliagiza Jeshi la Uhamiaji mkoani Mwanza kuchukua hati za kusafiria za wakandarasi wa kampuni ya Gas Entec Building Engineering wanaojenga meli hiyo kutokana na kushindwa kutekeleza matakwa ya mkataba.
Waziri Mkuu baada ya ukaguzi huo alibalini kuwa kampuni ambayo Serikali iliingia nayo mkataba ya GAS Entec iliuza share zake bila Serikali kuarifiwa na waliouziwa walipokuja walishangaa kuona ujenzi wa meli kwa sababu suala la ujenzi liko nje ya mauziano yao.
Mheshimiwa Majaliwa alisema Serikali imeshalipa asilimia 80 ya gharama za ujenzi wa meli hiyo lakini kazi iliyofanyika kwa mujibu wa mkataba ni asilimia 55 tu. Alisema taarifa alizonazo zinaonesha kuwa wafanyakazi walikuwa 118 lakini sasa wamebakia 22 tu.
“Haiwezekani tuwalipe hela hiyo, kazi haiendi kama ilivyopaswa. Tena wamepunguza Wafanyakazi kutoka 118 hadi 22, tunajuaje kama kesho watawaondoa hao 22 na wao wenyewe wapande ndege kurudi kwao, au waende Nairobi kupanda ndege,” alisema.
Naye, Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya amesema mkandarasi alirejea tena Mei 16, 2022 na kuendelea na utekelezaji wa mradi huo kufuatia maelekezo ya Waziri Mkuu aliyoyatoa Mei 7, 2022, ambapo wafanyakazi wote waliokuwa wamesitishiwa mikataba yao waliendelea na kazi.
Amesema kwa sasa ujenzi huo umefikia asilimia 73 na Novemba 30, 2022 itashushwa majini ili kumalizia kazi za mifumo ikiwa inaelea na kwamba ujenzi huo unatarajiwa kukamilika Mei 30, 2023. Meli hiyo inajengwa katika Ziwa Victoria kwa gharama ya shilingi bilioni 108, itakuwa na uwezo wa kuchukua abiria 1,200 na tani 400 za mizigo.
Kwa upande wake, Mbunge wa jimbo la Sumve, Kasalali Mageni akizungumza kwa niaba ya Wabunge wa mkoa wa Mwanza, ametumia fursa hiyo kumshukuru Mheshimiwa Rais Samia kwa kazi nzuri ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo anayoitekeleza mkoani hapa ikiwemo ujenzi wa meli ya MV Mwanza Hapa Kazi Tu.