Maandalizi ya maonesho ya Maadhimisho ya Kitaifa ya Juma la Elimu ya Watu Wazima 2022 yanaendelea katika viwanja vya Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE).
Maandalizi ya maadhimisho haya ya kitaifa yanaratibiwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Itakumbukwa kuwa maadhimisho ya Juma la Elimu ya Watu Wazima kimataifa hufanyika kila mwaka mwezi Septemba.
Nchini Tanzania maadhimisho haya huanzia katika ngazi ya Wilaya, Mkoa na hatimaye Kitaifa ambapo kwa mwaka huu yanafanyika kuanzia Oktoba 17-21, 2022 na yana kauli mbiu isemayo “Kuboresha Mazingira ya Kujifunza, Kusoma na Kuandika kwa kuzingatia Ubora, Usawa na Ujumuishi wa Makundi.”
Wadau mbalimbali wa Elimu ya Watu Wazima wakiwemo maafisa elimu ya watu wazima ngazi ya Mkoa, Halmashauri, Vyuo Vikuu, Uthibiti Ubora wa Shule na baadhi ya taasisi zilizo chini ya Wizara ambazo ni Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) na Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania (BOHUMATA) wanashiriki katika maonesho hayo.