Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Songea mkoani Ruvuma Neema Maghembe, akizungumzia juu ya ujenzi wa miundombinu ya elimu hususani bweni la wanafunzi wa shule za Sekondari Mpitimbi kata ya Mpitimbi ambapo Serikali imetumia kiasi cha Shilingi milioni 80 kumaliza tatizo la malazi kwa wanafunzi wa kike wa shule hiyo.
Bweni jipya lililojengwa na Serikali kupitia Halmashauri ya wilaya Songea mkoani Ruvuma likiwa limekamilika na kuanza kutumika na wanafunzi wa kike wa shule ya Sekondari ya Mpitimbi ambalo limegharimu Sh.milioni 80 ikiwa ni jitihada za Serikali ya awamu ya sita ya kuboresha na kuimarisha miundombinu ya elimu kwa shule mbalimbali hapa nchini.
Baadhi ya walimu na wanafunzi wa shule ya Sekondari Mpitimbi wakiwa katika picha ya pamoja.
moja kati ya vyumba vya madarasa vilivyojengwa na Serikali ya awamu ya sita kupitia Halmashauri ya wilaya Songea ambavyo vimesaidia sana kuongezeka kwa taaluma na kuhamasisha wanafunzi kuhudhuria masomo.
Picha na Muhidin Amri
…………………………………………
Na Muhidin Amri,Songea
WANAFUNZI wa shule ya Sekondari Mpitimbi Halmashauri ya wilaya Songea,wameishukuru serikali kupitia Halmashauri ya wilaya Songea kuwajengea bweni jipya na la kisasa lililo saidia kumaliza changamoto ya malazi na kupata muda wa kutosha wa kujisomea.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti walisema kuwa,jitihada za Halmashauri ya wilaya kuboresha miundombinu mbalimbali ikiwamo ujenzi wa bweni hilo na vyumba viwili vya madarasa vilivyojengwa kwa fedha za mpango wa maendeleo kwa ustawi wa jamii na mapambano dhidi ya Covid-19 ni kielelezo cha namna serikali ya awamu ya sita inavyowajali wananchi.
Salma Abdi mwanafunzi wa kidato cha tano alisema,awali walilazimika kulala kwenye bweni dogo na chakavu ambalo halikuwa salama kwa afya zao kutokana na sakafu yake kuwa ya udongo,hivyo kusababisha kutokea magonjwa ya mara kwa mara.
Alisema, baada ya kupata bweni jipya wanafunzi wa shule hiyo wataendelea kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan aliyedhihirisha nia yake ya kumkomboa mtoto wa kike kusoma kwa bidii.
Naye mwanafunzi mwingine Jackline Panaska,amemshukuru mbunge wa Jimbo la Peramiho Jenista Mhagama na wananchi wa kata ya Mpitimbi, kwa kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa bweni hilo na miundombinu mingine ya shule ambapo nguvu zao zimesaidia kupata bweni la kisasa ambalo ni mkombozi na kuhaidi kulitumia kuongeza muda wa kujisomea ili waweze kutumiza ndoto zao.
Aidha,ameiomba serikali kupitia wakala wa maji safi na salama(Ruwasa)wilaya ya Songea, kufikisha huduma ya maji hadi bwenini ili wayatumie kufanya usafi hasa kwenye vyoo ili kuwaepusha kupata magonjwa mbalimbali.
“tunaishukuru serikali yetu na mbunge wa jimbo letu mama yetu Jenista Mhagama kwa jitihada zake,hata hivyo tunaomba huduma ya maji safi na salama yafike bwenini kwa kuwa mazingira yetu yanahitaji maji mengi kutokana na wingi wa wanafunzi tuliopo”alisema.
Mwalimu wa ujenzi wa shule hiyo Mathew Haule alisema, walipokea jumla ya Sh.milioni 80 kutoka serikalini kwa ajili ya ujenzi wa bweni hilo ambapo fedha zilizotumika ni Sh. milioni 79,995.561 na kubaki shilingi 4,400.
Mwalimu Mathew alisema, hatua ya Serikali kujenga bweni kwa ajili ya wanafunzi wa kike imewasaidia wanafunzi hao kupata elimu bora na kuongezeka kwa taaluma ikilinganishwa na miaka ya nyuma.
Alisema,bweni hilo limejengwa mahususi kwa lengo la kuwasaidia wanafunzi wa kike wa kidato cha tano na sita kutoka katika makazi yao ili kufika shule kwa wakati na kuwawezesha kupata muda mwingi wa kujisomea na sehemu salama ya kuishi wakiwa shuleni.
“apo awali wanafunzi walitumia bweni dogo ambalo halikuwa salama kwa afya zao kwa kuwa chini kulikuwa na udongo,hivyo kusababisha kupata mafua mara kwa mara,tunaishukuru sana serikali kwa kujenga bweni jipya”alisema.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Songea Neema Maghembe alisema, kwa mwaka wa fedha 2021/2022 serikali imetumia jumla ya Sh.milioni 480 kwa ajili ya kujenga mabweni 6 katika shule za sekondari.
Aidha Maghembe alieleza kuwa, mwaka wa fedha 2022/2023 serikali imepanga kutumia Sh.milioni 320 kujenga mabweni mengine 4 ambapo wameshapokea Sh.milioni 160 kati ya Sh.milioni 320 kwa ajili ya kujenga mabweni 2.
Mkurugenzi huyo,ameishukuru serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuikumbuka Halmashauri hiyo kwa kuipa fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi na kuboresha huduma mbalimbali za kijamii.