Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, akimsikiliza Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mkoa wa Katavi, Eng. Martin Mwakabende, kuhusu hatua ya ujenzi wa barabara ya Kibaoni – Mlele Junction (km 50), kwa kiwango cha lami, Mkoani humo.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, akitoa maelekezo kwa Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mkoa wa Katavi Eng. Martin Mwakabende (kulia), wakati ujenzi wa barabara ya Kibaoni – Mlele Junction (km 50), kwa kiwango cha lami, Mkoani humo.
Muonekano wa sehemu ya barabara ya Kibaoni – Mlele (km 50) inayojengwa kwa kiwango cha lami, mkoani Katavi. Ujenzi wa barabara hiyo utagharimu Shilingi Bilioni 88.
PICHA NA WUU
……………………………..
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, ameelekeza ujenzi wa barabara ya Kibaoni – Mlele (km 50), kwa kiwango cha lami uanze katika Makao Makuu ya Halmashauri ya Mpimbwe kwa ajili ya kusogeza huduma za usafiri na usafirishaji wa abiria na mazao.
Prof. Mbarawa, ametoa agizo hilo mkoani Katavi, wakati alipokagua ujenzi wa mradi huo ulioanza kutekelezwa na mkandarasi China Railways Seventh Group na kusimamiwa na Kitengo Maalum cha Wahandisi Washauri (TECU) kwa gharama ya shilingi Bilioni 88 ambao utatekelezwa kwa muda wa miezi 36.
“Kikawaida Barabara inaanza kujengwa walipo wananchi na tumeshakubaliana na TANROADS mkoa kuwa wataanza kwa kuunganisha makao makuu ya halmashauri kwani kuna shughuli mbalimbali za kibinadam zinaendelea”, amesisitiza Prof. Mbarawa.
Prof. Mbarawa amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, kwa kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami na kufanikisha kuunganisha Wilaya ya Mlele na Mpanda ambapo kuna uzalishaji mwingi wa mazao ya mpunga, ufuta na mahindi.
Amewahakikishia wananchi wa Wilaya ya Mlele kuwa ujenzi wa barabara hiyo utakamilika kwa ubora unaotakiwa na kusisitiza kuwa mradi unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Juni, 2025.
Prof. Mbarawa ameahidi wananchi wa Mlele kupata ajira nyingi katika mradi huo na kuwaomba wale watakaopata fursa hiyo kuwa waaminifu na kuhakikisha wanatoa ushirikiano wakutosha kwa mkandarasi na kutohujumu mradi.
“Hii barabara ni yenu na mmeisubiri kwa muda mrefu sasa itakuwa jambo la ajabu kwa wale watakaopata kazi hapa kuanza kuiba mafuta au saruji, Tunataka barabara hii idumu kwa muda mrefu kama ilivyofanyiwa usanifu, hivyo tutunze vifaa na kushirikiana vyema na mkandarasi”, amefafanua Prof. Mbarawa.
Naye, Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Katavi, Eng. Martin Mwakabende amemueleza Waziri huyo kuwa mradi huo unahusisha usanifu wa kina pamoja na ujenzi na hatua zinazoendelea hadi sasa ni kwamba mkandarasi amekwishaleta mitambo eneo la kazi na kazi imeanza ya kusafisha barabara.
Ameeleza ujenzi wa kambi ya mkandarasi umekamilika kwa asilimia 100 na ujenzi wa kambi ya Mhandisi Mshauri na Maabara bado inaendelea.
Waziri Prof. Mbarawa yupo mkoani Katavi ambapo amekagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na Wizara ikiwemo miundombinu ya barabara.