Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameziagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU) na Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA) kufuatilia miradi ya maendeleo iliyobainika kuwa na dosari.
Rais Samia ametoa agizo hilo leo kwenye hafla ya Maadhimisho ya Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru 2022 na kumbukumbu ya Baba wa Taifa hayati Mwalimu Julius Nyerere iliyofanyika katika Uwanja wa Kaitaba.
Aidha, Rais Samia amezitaka TAKUKURU na ZAECA kuwachukulia hatua wasimamizi wa miradi iliyobainika kuwa na ufujaji, wizi, matumizi mabaya ya fedha, pamoja na rushwa.
Rais Samia pia amesema vitendo vya rushwa vinajirudia kwa kuwa Viongozi katika maeneo mbalimbali hawafuatilii maendeleo ya miradi ya wananchi hadi Mwenge wa Uhuru unapopita na kubaini dosari hizo katika miradi hiyo.
Vile vile, Rais Samia amewataka Viongozi na watendaji wahakikishe wanasimamia matumizi sahihi ya fedha zinazoelekezwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Rais Samia pia amekemea tabia ya baadhi ya viongozi wasiojali na kuhurumia wananchi kwa kuwapa miradi Wakandarasi wasio na uwezo na kusababisha miradi kutotekelezwa ipasavyo.
Mbio za Mwenge wa Uhuru zilizinduliwa tarehe 02 Aprili, 2022 ambapo miradi ya maendeleo 1293 iliyogharimu shilingi bilioni 650.8 ilizinduliwa na kuwekwa mawe ya msingi katika maeneo mbalimbali hapa nchini.