Viongozi na wachezaji wa Klabu za Michezo mbalimbali wanachama wa Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) wakikabidhi misaada mbalimbali ya vyakula na fedha kwa watoto wenye uhitaji inayosimamiwa na Watawa wa Shiriki la Collegine wa Familia Takatifu katika Nyumba ya Furaha iliyopo Raskazon Jijini Tanga. Msaada huo uliopokelewa na Mlezi wa kituo hicho Sr. Irene Kafuka (aliyebeba mtoto mchanga) ni sehemu ya msaada wa kijamii unaotolewa na SHIMIWI ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Kumbukumbu ya Baba wa Taifa Mwl. Julius Nyerere.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI), Alex Temba akiwakabidhi baadhi ya Wazee wa Nyumba ya Wazee kiasi cha Tshs. Milioni 1 pamoja na misaada mbalimbali ya vyakula wanaoishi katika Makao ya Kulea Wazee Wasiojiweza Mwanzange Jijini Tanga. ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Kumbukumbu ya Hayati Baba wa Taifa Mwl. Julius Nyerere.
Katibu Mkuu wa wa Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) Alex Temba (kulia aliyebeba mtoto) akimkabidhi Mlezi wa Nyumba ya Furaha inayosimamiwa na watawa wa Collegine wa Familia Takatifu, Sr. Irene Kafuka (kushoto) mahitaji muhimu kwa binadamu na fedha taslim zilizotokana na michango ya wanamichezo wanaoshiriki michezo ya 36 ya SHIMIWI inayofanyika Jijini Tanga ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Kumbukumbu ya Hayati Baba wa Taifa Mw. Julius Nyerere
…………………………………..
Na Mwandishi Wetu, Tanga
WAKATI michezo ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) itahitimishwa Oktoba 15, 2022 kwa kufungwa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Omar Mgumba, timu 64 Oktoba 14, 2022 zimefanya matendo ya huruma kwa kurudisha kwa watu wenye uhitaji kwa kuwanunua mahitaji muhimu ya binadamu na kuwapa fedha taslim.
Katika ufungaji huo timu zitakazocheza fainali katika mchezo wa soka ni Idara ya Mahakama kuumana na Hazina kutoka Wizara ya Fedha na Mipango; huku katika netiboli wataumana Ofisi ya Rais Ikulu dhidi ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) na katika kamba wanawake watacheza Sekta ya Uchukuzi dhidi ya Idara ya Mahakama; na wanaume Ofisi ya Rais Ikulu na Idara ya Mahakama.
Kwa upande wa Vituo vilivyopata misaada ni Chuo cha Ufundi na Marekebisho kwa Watu wenye Ulemavu Masiwani; Makao ya Wazee Wasiojiweza Mwanzange na Nyumba ya Furaha inayohudumiwa na Watawa wa Shirika la Collegine wa Familia Takatifu, ambapo Katibu Mkuu wa SHIMIWI, Alex Temba amesema wamefanya matendo haya wakimuenzi Hayati Baba wa Taifa, Julius Kambarage Nyerere, ambapo watumishi wanaoshiriki kwenye michezo ya SHIMIWI wamekuwa na desturi ya kutenga siku moja, kwa ajili ya kujumuika na vituo vya wahitaji vilivyoteuliwa katika kituo cha mashindano na kutoa misaada mbalimbali ya kibinadamu.
“Tunashukuru Mungu Serikali imetupa kibali cha kushiriki kwenye michezo ya SHIMIWI, nasi hatuna budi kujumuika na wenzetu wenye uhitaji kwa kurudisha tulichopata ili kuwaonesha upendo tulionao kwao na hii ni tabia yetu kila tunapofanya mashindano yetu kwa kusaidia kwenye mkoa ambao mashindano yanafanyikia,” amesema Temba.
Naye Mratibu wa zoezi hili, Itika Mwankenja amesema wamekusanya kiasi cha Tshs. Milioni 4.5 ambazo zimetumika kununulia vyakula kama mchele, maharage, unga, sukari, chumvi, mafuta ya kula, sabuni za kufulia na kuogea, mafuta ya kujipaka, maji katoni 100, juisi, dawa za meno, miswaki, nepi maalum za watoto wadogo, madaftari, penseli, raba na fulana za kike.
Halikadhalika wamechangia bima za afya kwa Watoto watano na pia kutoa fedha taslim kiasi cha Tshs. Milioni 3.3 kwa kituo kimoja kumepewa Tshs. Milioni 1.3 na vingine viwili vimepewa Tshs. Milioni 1 kwa kila kimoja.
Wakishukuru kwa nyakati tofauti baada ya kupokea misaada hiyo, Kaimu Mkuu wa Chuo cha Ufundi na Marekebisho kwa Watu wenye Ulemavu Masiwani, Bi. Mwantumu Zayumba amesema kituo anachokisimamia kinawatoto 60 wenye ulemavu wa usikivu, macho, mabubu na ulemavu wa viungo mbalimbali ambao kwa sasa wanaotokea majumbani huku wa kulala mabwenini wataanza Januari 2023, na sasa wanajifunza shughuli mbalimbali zikiwemo za ushonaji wa nguo.
Kwa upande wake Afisa Ustawi wa Jamii na Kaimu Mkuu wa Nyumba ya Wazee Wasiojiweza, Bw. Emmanuel Joseph pamoja na kushukuru kwa misaada mbalimbali waliyopata amesema nyumba hiyo inawazee 17 miongoni mwao wanaume ni 14 na wanawake watatu.
Akishukuru kwa niaba ya wazee wenzake, Mzee Isdor Dismas ambaye ni shabiki kindakindaki wa Yanga, amewashukuru watumishi kwa kuwakumbuka kwa misaada mbalimbali na anawaombea kwa Mwenyezi Mungu waendelee na moyo huo wa kutoa kwa jamii zenye uhitaji.
Naye Mlezi wa Nyumba ya Furaha inayosimamiwa na watawa wa Collegine wa Familia Takatifu, Sr. Irene Kafuka amesema kituo hicho kinawatoto zaidi ya 70 na hakina mfadhili zaidi ya kupata misaada kutoka kwa wasamaria wema, ambapo lengo kuu ni kuokoa maisha ya watoto ambao wanaletewa kutoka ustawi wa Jamii, wakiwemo waliotelekezwa.
“Hatuchukui watoto huko mitaani, ila sisi tunaletewa na maafisa kutoka Ustawi wa Jamii na watoto tunaowalea hapa ni zaidi ya yatima asilimia kubwa hawana ndugu na mtoto mdogo kabisa anamiezi mitano, ingawa wapo wakubwa waliokulia hapa na sasa wapo chuoni na kwa kuwa hawana ndugu hapa ndio nyumbani kwao tunaendelea kuishi nao tukishikiana na watawa wengine tupo watawa nane,” amesema Sr. Irene.
Hata hivyo, Sr. Irene amesema wakiwa kama watawa wanauvaa ualisia wa umama na kujitoa kwa moyo kulea watoto hao wadogo kama usemi wao unavyosema “Upendo ni kujitoa bila kipimo”.