**************************
Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha
Oct 14
JUMLA ya mabinti 142 waliokatishwa masomo yao kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kupata mimba Mkoani Pwani ,wamesajiliwa katika program ya elimu Sekondari kwa njia mbadala (SEQUIP) ,iliyoanzishwa na Rais Samia Suluhu Hassan ili kuwaendeleza mabinti hao waweze kutimiza ndoto zao.
Kati ya idadi hiyo mabinti waliobakia Ni 130 ambapo kati yao 14 pekee wapo Halmashauri ya Mji Kibaha .
Akizungumza katika maadhimisho ya kilele Cha Juma la Elimu ya watu wazima Halmashauri ya Mji wa Kibaha, Katibu Tawala wilaya ya Kibaha,Sozi Ngate alieleza, kufuatia taarifa hizo inaonyesha mwamko bado ni mdogo ,Kuna kila sababu ya kuunga mkono juhudi za Serikali ili watoto hao wapate elimu ngazi ya Sekondari.
Alitoa wito kwa jamii na viongozi kuhamasisha kuwapeleka mabinti hao wenye umri kati ya miaka 13-20 kujiunga na program hiyo ili kujiendeleza na kutimiza ndoto zao.
“Namshukuru Rais wetu Samia Suluhu Hassan kwa kuona umuhimu wa wasichana waliokatishwa masomo kwa sababu mbalimbali ikiwemo mimba, Ukosefu wa ada kurudi shuleni, Serikali imeanzisha program hii inayoitwa Sequip , mradi ambao ni wa Serikali chini ya Taasisi ya elimu ya watu wazima inayoendesha mafunzo ya elimu ya Sekondari kwa wasichana wenye umri kati ya miaka 13-20”
Vilevile , aliwaasa wazazi na walezi kuwapeleka watoto wao ambao hawakupita kwenye mfumo rasmi yaani kusajiliwa kwa wa kuanza shule ya msingi waandikishwe MEMKWA.
“Wazazi msikae na watoto nyumbani wapelekeni shule,msisite kwakuwa wamechelewa kwenda shule, kwani Serikali imeleta mpango MEMKWA ili kuwasaidia watoto hao wapate haki yao ya elimu.”alisisitiza Sozi.
Hata hivyo alitoa rai, vijana wasiachwe mitaani hata watu wazima wenye miaka 60-70-80 wanaotaka kujiendeleza wasisite kutumia fursa ya mpango wakujiendeleza watu wazima (MUKEJA).
Nae mkufunzi Taasisi ya Elimu ya watu wazima Binuru Kivaria alisema bado Kuna mahitaji ya mabinti 140 katika mpango wa SEQUIP kwenye Halmashauri ya Mji Kibaha ambapo kwasasa wapo 14 pekee .
“Tuleteeni mabinti hawa ,hawa 14 mliowaona ni idadi ndogo sana ,kimkoa wapo 130 waliobaki kutokana na changamoto mbalimbali ambapo mwanzo tuliwasajili 142′;alisema Binuru.
Awali ofisa elimu ya watu wazima Halmashauri ya Mji wa Kibaha, Juliana Mwakatenya, alieleza hali ya elimu ya watu wazima kwenye Halmashauri hiyo siyo ya kuridhisha.
“Baadhi ya vikwazo vinavyochangia kuzorota kwa shughuli za elimu ya watu wazima ni upungufu wa walimu wenye ujuzi wa kufundisha watu wazima, Ukosefu wa vifaa,maudhurio hafifu ya wanakisomo kutokana na kusongwa na shughuli za kujikimu kimaisha”alifafanua Mwakatenya.
Mwanafunzi aliye katika mpango wa SEQUIP shule ya Sekondari Tumbi, Blandina Lukosi alisema ,alikatishwa masomo yake ya Sekondari na kijana ambae alimpa mimba hali iliyopelekea kukatisha ndoto zake.
Alisema ,baada ya kusikia mpango huo ulioanzishwa na Rais Samia Suluhu Hassan anamshukuru kwani ameweza kujiendeleza kimasomo.
Blandina alitaja changamoto zinazowakabili katika mpango huo ni pamoja na watu kuwakatisha tamaa na kuwaita wazazi na sio wanafunzi,kupewa jina la wanafunzi wa Samia .
“Tunaomba msaada wa bweni ,ambalo litatusaidia kupata muda mwingi wa kujisomea ,muda tulipewa ni mfupi ,pia tatizo la nauli ,tunaomba tuwezeshwe ili kusije kupata changamoto Kama za awali”
Kwa upande wake, Mzee wa miaka 70 ,Hussein Rashid alisema amepata elimu ya watu wazima ,anashukuru Sasa anajua kusoma na anatumia simu kiganja vizuri wakati zamani alikuwa akisomewa na wajukuu zake.
“Kilichonifikisha hapa miaka hiyo tulikuwa hatuingii shuleni hadi mkono ufike sikioni,sasa mimi nilipoona mkono haujafika sikioni nikaacha nikawa nawinda ndege mashambani na kulima,”alieleza mzee Hussein.
Picha mbalimbali za Juma la maadhimisho ya elimu ya watu wazima Halmashauri ya Mji Kibaha…