Prof. Youjin B. Chung, kutoka Chuo Kikuu Cha California –Berkeley, akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili Chuo Kikuu Mzumbe, Kampasi Kuu Morogoro.
Kaimu Mkurugenzi wa Mahusiano ya Kimataifa na Baraza la Wahitimu, Dkt. Lucy massoi (Kushoto), akizungumza katika kikao cha ukaribisho. Kulia ni Prof. Youjin B. Chung, kutoka Chuo Kikuu Cha California- Berkeley.
Viongozi wa Menejimenti wakimsikiliza, Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. William Mwegoha, katika kikao kilichofanyika Chuo Kikuu Mzumbe, Kampasi Kuu Morogoro.
Prof. Youjin B. Chung, kutoka Chuo Kikuu Cha California- Berkeley, akizungumza na viongozi wa Chuo Kikuu Mzumbe.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. William Mwegoha (Kushoto), akimkabidhi zawadi Prof. Youjin B. Chung, kutoka Chuo Kikuu Cha California- Berkeley.
Prof. Youjin B. Chung, kutoka Chuo Kikuu Cha California, Berkeley (Katikati) akiwa na viongozi wa Menejimenti wa Chuo Kikuu Mzumbe.
……………………………………..
Chuo Kikuu Cha California – Berkeley, Marekani, kimeanzisha mahusiano na ushirikiano na Chuo Kikuu Mzumbe, ili kuimarisha na kukuza taaluma katika maeneo bobevu hususani maendeleo ya sayansi ya mazingira, utawala, sera na usimamizi.
Akizungumza wakati wa kikao na Makamu Mkuu wa Chuo Prof. William Mwegoha, Prof. Youjin B. Chung, Mtaalamu wa maendeleo ya sayansi ya mazingira, sera na usimamizi kutoka Chuo hicho amesema wamevutiwa na maeneo ya ubobevu na tafiti yanayotolewa na Chuo Kikuu Mzumbe na hivyo kuanzisha ushirikiano huo ni muhimu na bora baina ya vyuo hivyo kwani utasaidia kukuza maeneo ya utafiti na taaluma.
Akizungumza katika kikao hicho, Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. William Mwegoha, amesema Mzumbe ni sehemu sahihi na bora ya kuanzisha, kukuza na kuendeleza ushirikiano katika maeneo ya ubobevu wa kitaaluma na tafiti na kwamba Chuo Kikuu Mzumbe kiko tayari kutoa ushirikiano katika kuhakikisha malengo ya ushirikiano baina ya vyuo hivyo yanafikiwa.
Akielezea hatua za ushirikiano huo, Kaimu Mkurugenzi wa Mahusiano ya Kimataifa na Baraza la Wahitimu, Dkt. Lucy massoi , amesema wamejizatiti kuhakikisha ushirikiano na taasisi za kimataifa zinazohusu tafiti na masuala ya elimu ya juu unaanzishwa na kuendelezwa, na kwamba tayari wameandaa mkataba wa mashirikiano na chuo cha Berkeley ambao unaonyesha maeneo ya ushirikiano, na utasainiwa wakati wowote ukisharidhiwa na pande zote.
Kikao cha Utambulisho na maridhiano kilifanyika Chuo Kikuu Mzumbe Kampasi Kuu Morogoro na kuhudhuriwa na baadhi ya wajumbe wa Menejimenti ya Chuo hicho.