Mkuu wa mkoa wa Arusha ,John Mongela akizindua rasmi kituo cha ujasiriamali na ubunifu kwa vijana cha Westerwelle Startup Arusha
Baadhi ya washiriki wakishuhudia uzinduzi wa kituo hicho kipya ya ujasiriamali na ubunifu kwa vijana katika hafla iliyofanyika mjini hapa.
……………………………..
Julieth Laizer,Arusha
Zaidi ya vijana 150 kutoka maeneo mbalimbali mkoani Arusha wamenufaika na kituo cha ujasiriamali na ubunifu cha Westerwelle Startup Haus Arusha kwa kupatiwa elimu kuhusu maswala ya ujasiriamali na kuunganishwa na masoko ndani na nje ya nchi.
Hayo yamesemwa jijini Arusha na Meneja Mkuu wa kituo hicho cha Westerwelle Startup Haus Arusha,Collins Kimaro wakati akizungumza katika uzinduzi wa kituo hicho uliofanyika jijini Arusha.
Amefafanua kuwa, Westerwelle Foundation kutoka Ujerumani imeungana na Obuntu Hub kutoka Arusha kufungua kituo hicho kikubwa kwa ajili ya kuwasaidia vijana wajasiriamali Tanzania na kuweza kuanzisha shughuli zao na kuondokana na changamoto ya ukosefu wa ajira.
Kimaro amesema kuwa,uzinduzi wa kituo hicho cha ujasiriamali na ubunifu kwa vijana kinalenga kuwasaidia vijana wajasiriamali Tanzania kwa lengo la kuchochea maendeleo kupitia ujasiriamali.
Amesema kuwa,Tanzania sasa inajiunga kwenye mtandao huo wa kimataifa ambao tayari kuna kituo Tunisia,Rwanda,ambapo malengo yao ni kuongeza nchi moja kila mwaka.
Ameongeza kuwa, kituo hicho tayari kina programu 4 kwa ajili ya wajasiriamali kwenye sekta za kilimo,utalii,uchumi wa kidigitali na mabadiliko ya tabia nchi kukiwa na lengo la kufikia vijana 5,000 ndani ya miaka mitano ijayo.
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Arusha,John Mongela akizungumza katika uzinduzi huo amesema kuwa ,uwepo wa kituo hicho utasaidia sana kuwaunganisha vijana na masoko ndani na nje ya nchi na kuweza kuanzisha biashara zao na kuondokana na changamoto ya ajira.
Mongela amewataka vijana hao kutumia kituo hicho kupata fursa mbalimbali kujikwamua kiuchumi na kuweza kuondokana na changamoto mbalimbali z ajira.
Amesema kuwa,kituo hicho kwa Arusha kinatoa mafunzo kwa vijana wabunifu na wajasiriamali katika kuwapa nafasi za kufanyia shughuli zao na kuwasaidia kupata rasilimali mbalimbali.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa bodi ya Westerwelle Foundation ,Michael Mronz amesema kuwa wamefungua kituo hiki nchini Tanzania kwa lengo la kuwawezesha vijana kuweza kunufaika na fursa nyingi .
Mronz amesema kuwa, Tanzania ina fursa nyingi kutokana na uchumi unaokuwa kwa kazi,nguvu kazi kubwa,utulivu wa kisiasa, na serikali yenye ushirikiano mkubwa.
“Vituo hivi vinalenga kuwasaidia vijana kuweza kuwa wabunifu na kuendeleza bunifu zao sambamba na kuwatafutia masoko ndani na nje ya nchi na vijana wengi wameweza kunufaika na kituo hiki kwani kipo nchini Kigali,Tunisia na Tanzania hapa Arusha,hivyo nawaomba sana vijana wajitokeze kwa wingi kuchangamkia fursa mbalimbali kupitia kituo hiki cha kusaidia vijana katika maswala mbalimbali.”alisema Mronz.
Baadhi ya vijana wanaonufaika na kituo hicho ,Getruda Mollel amesema kuwa, kupitia kituo hicho wameweza kunufaika kwa kuanzisha shughuli mbalimbali sambamba na kupata fursa ya kuunganishwa na masoko ya nje ya nchi na kuwez kujikwamua kiuchumi.