Afisa masoko wa Shirika la viwango Tanzania (TBS) Roda Mayugu wa kushoto akitoa maelezo kwa Naibu waziri wa Wizara na uwekezaji na biashara Exavd Kigahe alipotembelea banda hilo.
……………………………
Na Victor Masangu,Pwani
Shirika la viwango Tanzania (TBS) katika kuwajengea mazingira limejipanga kuwatembelea wafajasiriamali wadogo pamoja na wakubwa kwa ajili ya kuwaelimisha zaidi kuhusuana na kutengeneza bidhaa zao kwa kiwango kinachotakiwa.
Hayo yamebainishwa na Afisa masoko wa TBS Roda Mayugu wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu yao kwa Naibu waziri wa Wizara ya uwekezaji na biashara ambaye alitembelea banda hilo wakati wa wiki ya maonyesho yaliyofanyika Wilayani Kibaha Mkoani Pwani.
Afisa huyo alibainisha kwamba kwa Sasa wanajipanga kwa ajili ya kufanya ziara ya kuwatembelea wajasiriamali katika maeneo yao ambayo wanafanyia kazi ikiwemo katika maeneo mbali mbali ikiwemo sokoni.
“Kwa Sasa Shirika letu tumeona ni vizuri tukaboresha zaidi huduma zetu kwa kwenda kuwaona wahusika mpaka uko masokoni na kuwapa elimu ambayo itawasaidia katika kuboresha bidhaa zao ziwe katika kiwango kinachotakiwa,”alisema afisa huyo.
Pia aliwaomba wafanyabiashara wakubwa pamoja na wale wajasiriamali wadogo kutengeneza bidhaa zao kwa kiwango kinachotakiwa ili ziweze kupata soko na kuuzika ndani na nje ya nchi kutokana na kuwa na ubora.
“Shirika letu la TBS linafanya kazi katika ubora unaotakiwa na kwamba tupo katika Kanda zipatazo saba ikiwemo mikoa ya Dodoma,Dar es Salaam,Mwanza,Arusha,Mbeya na dhamira yetu ni kuwafikia kwa ukaribu na suala la kudhibitisha ubora wa bidhaa ni bure,”alisema Roda.
Awali Naibu Waziri wa uwekezaji na biashara Exavd Kigahe alipotembelea banda hilo aliwapongeza TBS kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kudhibiti ubora wa bidhaa zinazozalishwa.
Aliongeza kuwa kunatakiwa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara ambao utasaidia kubaini changamoto zilizopo katika bidhaa ili ziweze kufanyiwa kazi na kutafutiwa ufumbuzi.