JESHI la Polisi Mkoa wa Mwanza limeendelea na operesheni mbalimbali za kupambana na uhalifu na wahalifu kwenye maeneo ya nchi kavu na majini kwa nia ya kuendeleza kudhibiti hali ya utulivu ndani ya Mkoa.
Katika operesheni za nchi kavu, Jeshi la Polisi lilifanikiwa kukamata simu 118 na watuhumiwa 8 waliokuwa wanajihusisha na ukwapuaji/uporaji wa simu katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Mwanza. Mafanikio haya ni kutokana na ushirikiano wa wananchi uliowezesha kumkamata mtuhumiwa aliyekuwa anapokea na kununua simu za wizi toka kwa watuhumiwa wa wizi wa simu hizo.
Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama limefanikiwa kukamata injini 4 za boti, nyavu haramu na watuhumiwa wa makosa mbalimbali ya uvuvi haramu ndani ya Ziwa Victoria na kwa upande wa barabarani makosa mbalimbali yameendelea kudhibitiwa na mengine yamekamatwa na kutozwa faini kiasi cha Tshs 360,167,500/= ambazo zimeingizwa kwenye mfuko wa serikali.
Hata hivyo, mapambano dhidi ya dawa za kulevya bado yanaendelea ambapo Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa 8 wa makosa mbalimbali yanayohusiana na dawa za kulevya na watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani kukabiliana na mkono wa sheria.
Aidha, Katika tukio lingine tarehe 9 Oktoba 2022 majira ya 16:45 Jioni, huko maeneo ya hifadhi ya Msitu wa Sayaka uliopo Kata ya Itumbili, Wilaya ya Magu. Mwanamke mmoja ambaye jina lake linahifadhiwa alikutwa amekatwa sehemu zake za siri pamoja na chuchu za matiti yake yote mawili na mtu aliyetambulika kwa jina moja la Masoud, ambaye inadaiwa alikuwa mpenzi wake waliyedumu naye kwa muda wa miezi miwili.
Uchunguzi wa awali umebaini chanzo cha tukio hilo ni imani za kishirikina ambapo mtuhumiwa alimuadaa Mhanga kuwa anaenda kumuonyesha Shamba la dengu lililopo katika msitu wa hifadhi ya Sayaka na walipofika alimkaba shingoni Mhanga huyo ambapo ilipelekea kupoteza fahamu na kutekeleza unyama huo.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linafanya kila jitihada kuhakikisha linamtia nguvuni mtuhumiwa huyo ili aweze kufikishwa katika vyombo vya dola. Mhanga wa tukio hilo anaendelea kupatiwa matibabu katika hospitali ya rufaa Bugando na hali yake inaendelea vizuri.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linatoa wito kwa wananchi wote kuendelee kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu ili ziwezekufanyiwa kazi kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu.
Imetolewa na;-
Ramadhani H. Ng’anzi – SACP.
Kamanda wa Polisi (M) Mwanza.