Mkemia Mkuu wa Serikali, Dk.Fidelice Mafumiko,akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Utekelezaji wa Shughuli mbalimbali za Mamlaka hiyo na mwelekeo wa utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2022/2023 leo Oktoba 11,2022 jijini Dodoma.
…………………………….
Na Alex Sonna-DODOMA
MAMLAKA ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali imetaja vipaumbele mbalimbali vya mwaka 2022/23, ikiwamo kununua mitambo na vifaa vya kisasa pamoja na kuimarisha miundombinu ya uchunguzi wa kimaabara.
Hayo yameelezwa leo Oktoba 11,2022 jijini Dodoma na Mkemia Mkuu wa Serikali, Dk.Fidelice Mafumiko,wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Utekelezaji wa Shughuli mbalimbali za Mamlaka hiyo na mwelekeo wa utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
Dk.Mafumiko amesema kuwa Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 22 kwaajili ya kutekeleza na kuimarisha kwa kukamilisha ujenzi wa Jengo la Ofisi na Maabara la Makao Makuu ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali jijini Dodoma.
”Fedha hizo zitatumika kununua mitambo na vifaa vya kisasa vya kimaabara kwa ajili ya kuendelea kuboresha uchunguzi wa kisayansi wa kimaabara kwa lengo la kusimikwa kwenye Jengo la Mamlaka Makao Makuu ya Nchi-Dodoma.”amesema Dk.Mafumiko
Amesema katika Mwaka wa Fedha 2021/22 vibali vya uingizaji wa kemikali viliongezeka kufikia 63,588 ikilinganishwa na vibali 49,234 vilivyotolewa Mwaka wa fedha 2020/21 ikiwa ni ongezeko la vibali 14,354.
“Mbali na utoaji vibali vya kemikali, Mamlaka katika kipindi cha Mwaka wa Fedha 2021/22 imefanikiwa kusajili wadau wanaojihusisha na shughuli za kemikali 1087 ikilinganisha na wadau 1057 waliosajiliwa kwa Mwaka Fedha 2020/21 ikiwa ni ongezeko la wadau 30,”amesema Dk.Mafumiko
Dk.Mafumiko amesema kuwa vipimo vya vinasaba (DNA) ameeleza kuwa uhalisia wa kipimo hicho gharama yake ni Sh.700,000 hadi 800,000 kutokana na ughari wa kemikali lakini kwa muda mrefu serikali imebeba gharama hizo ili wananchi wapate huduma.
“Zile kemikali zinazosaidia kufanyika kipimo ni za ghari na kuna kemikali moja huwa tunanunua kila baada ya miezi mitatu ni Dola za Marekani 6,000 lakini ikitokea suala la janga huisha kabla ya muda huo,”amesema
Hata hivyo amesema kuwa kama mtu anataka kupima vinasaba vya baba, mama na mtoto ni Sh.300,000 na wamepeleka mapendekezo serikalini iongezeke kidogo ili kusaidia kuhudumia watu bila kuathiri uendeshaji wa mitambo na gharama za kemikali.
“Sehemu kubwa ya DNA inatumika kwenye masuala ya jinai kama masuala ya ulawiti, ubakaji, au hata wizi, kwa hiyo sio kwamba DNA inatumika kuonesha wazazi halisi lakini inasaidia kwenye masuala hayo ya jinai,”amesisitiza
Aidha Dk.Mafumiko amesema kuwa Serikali kupitia Mamlaka imepanga Kuimarisha biashara ya kemikali kwa kuendelea kuboresha usimamizi wa uingizaji wa kemikali nchini kwenye maeneo ya mipakani.
“Katika kutekeleza hilo, Mamlaka itaendelea kutoa huduma za ukaguzi wa shehena za kemikali katika maeneo yote ya mipakani kwa saa 24, siku saba kwa wiki”amesema
Amesema kuwa Mamlaka itaendelea na utaratibu wa kuimarisha Mfumo wa utoaji vibali vya uingizaji wa shehena za mizigo ya kemikali inayotarajiwa kuingizwa nchini.