*************************
Mwandishi wetu, Arusha.
WANAFUNZI wa shule ya msingi Prestige ya jijini Dar es salaam, wameeleza maajabu ya vivutio vya utalii vilivyopo nchini na kushauri watoto wa shule nyingine kupatiwa nafasi ya kutembelea hifadhi za Taifa na maeneo ya vivutio vya utalii.
Wakizungumza na waandishi wa habari, wakiwa kwenye kituo cha Utalii cha Cultural Heritage jijini Arusha, baada ya kutembelea Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro, hifadhi ya Taifa ya Tarangire na hifadhi ya Taifa ya Manyara, wanafunzi hao wameeleza kuona maajabu mengi katika hifadhi hizo.
Wanafunzi Kenzi Lewanga, Jaden James, Diana Komu, Illa Munisi na Ebeneza Charles wamesema hawakuwahi kuona kama Tanzania imejaliwa kuwa na wanyama wengi wa aina mbalimbali, ndege na mazingira mazuri ya kuvutia.
“Kuna maajabu mengi tumeona ndani ya bonde la Ngorongoro, eneo la Olduvai George na makundi makubwa ya tembo katika hifadhi ya Taifa ya Tarangire,” amesema Lewanga.
Mwanafunzi Diana Komu amesema wameshuhudia katika hifadhi ya Taifa ya Manyara, simba wakiwa wanapanda miti huku pia kukiwa na wanyama wengi.
Munisi amesema wakiwa katika kituo cha Tanzanite Cultural Heritage wamepata elimu ya asili na historia na maisha ya wale wa kale, michezo ya wanyama na vitu vya asili.
“Tumepata elimu nzuri, tumejifunza vitu vingi na maswali haya huwa tunaulizwa shuleni kwenye mitihani na sasa tumejionea wenyewe,” amesema.
Mwalimu wa shule hiyo, Dorice Brown amesema shule hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam, iliamua kuwapeleka wanafunzi hao kujifunza kwa vitendo vivutio vya utalii na rasilimali za taifa katika hifadhi.
“Tumetembelea hifadhi za Taifa na hapa katika kituo cha Tanzanite Cultural Heritage wamejifunza historia nzuri ya binaadamu na vitu vya asili,” amesema.
Wanafunzi 25 wa shule hiyo ambao wanasoma darasa la tano wameahidi kuwa mabalozi wa utalii wa Tanzania mara baada ya kurejea shuleni.