Na Shamimu Nyaki
Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul ameeleza kuwa wizara yake na Maliasili na Utalii zimekubaliana kushirikiana katika kuandaa matamasha ya Utamaduni ili kutangaza Utalii wa Kitamaduni.
Naibu Waziri Gekul, amesema hayo Oktoba 07, 2022 wakati akizindua Tamasha la Maasai Festival jijini Arusha ambalo linatarajiwa kuanza kufanyika mwaka 2023.
“Tutakua na kalenda ya pamoja na wizara ya Maliasili na Utalii ya matukio na matamasha ya Utamaduni ili yaweze kutumika katika Utalii na kuitangaza nchi” amesema Mhe. Gekul.
Mhe. Gekul ameziagiza Idara za Utamaduni na Sanaa kufanya tafiti na kuhifadhi kumbukumbu za makabila pamoja kukuza Matumizi ya lugha ya Kiswahili, huku akisisitiza wadau wengi kujitokeza kuunga mkono shughuli hizo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mhe.Saidi Mtanda amesema Utamaduni na Utalii unashabihiana hivyo vinayo nafasi kubwa katika kutangaza nchi.
Naye Muandaaji wa Tamasha hilo Bw. Saidi Rukemo ameeleza kuwa lengo la Tamasha hilo ni kuunga mkono jitihada za Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan za kutangaza nchi, ambapo amesema kupitia kabila la Wamasai kuheshimu na kutunza mila, Desturi na tamaduni zao itasaidia kurithisha kwa makabila na jamii nyingine.
Tamasha hilo linatarajiwa kufanyika mwezi wa nane mwaka 2023na linatarajiwa kuwa na wageni takriban 1500 wa ndani na nje ya nchi, ambalo litatawaliwa na burudani, fursa za kibiashara katika Utalii wa Utamaduni na kuvutia watalii wengi.