Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji akimsikiliza Meneja wa Idara ya Mawasiliano Benki Kuu ya Tanzania(BoT) Bi. Vick Msina alipokuwa akitoa maelezo wakati waziri huyo alipotembelea banda la benki hiyo kwenye maonesho ya 5 ya teknolojia ya Madini yaliyofungwa leo kwenye viwanja vya EPZA Bombambili mkoani Geita kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Geita Martin Shigella na katikati ni Waziri wa Madini Dkt. Dotto Biteko.
Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji akimsikiliza Meneja Msadizi Akiba ya Fedha za Kigeni wa Benki kuu ya Tanzania (BoT) Dkt. Anna Lyimo alipokuwa akitoa maelezo wakati waziri huyo alipotembelea banda la benki hiyo kwenye maonesho ya 5 ya teknolojia ya Madini yaliyofungwa leo kwenye viwanja vya EPZA Bombambili mkoani Geita wa pili kutoka kulia ni Waziri wa Madini Dkt. Dotto Biteko, Mbunge wa jimbo la Greita mjini Mh. Constantine Kanyasu na Meneja wa Idara ya Mawasiliano Benki Kuu ya Tanzania(BoT) Bi. Vick Msina.
Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji akiuliza jambo kwa Meneja Msadizi Akiba ya Fedha za Kigeni wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Dkt. Anna Lyimo katikati ni Meneja wa Idara ya Mawasiliano Benki Kuu ya Tanzania(BoT) Bi. Vick Msina alipokuwa akitoa maelezo wakati alipotembelea banda la benki hiyo.
Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji akimkabidhi Mkurugenzi wa Benki Kuu tawi la Mwanza Dkt. James Machemba Tuzo ya mshindi wa pili kwa taasisi za kifedha baada ya benki hiyo kushinda katika maonesho ya 5 ya teknolojia ya madini yaliyomalizika leo kwenye viwanja vya EPZA Bombambili mkoani Geita wanaoshuhudia katikati ni Waziri wa Madini Dkt. Dotto Biteko na kushoto ni Mkuu wa mkoa wa Geita Martin Shigella.
Mmoja wa wananchi waliotembelea banda hilo akiwauliza maofisa wa benki hiyo namna anavyoweza kutunza noti yake ya shilingi elfu 10.000.
Meneja wa Idara ya Mawasiliano Benki Kuu ya Tanzania(BoT) Bi. Vick Msina akijadiliana jambo na Katibu Tawala wa mkoa wa Geita Prof. Godius Kahyarara alipotembelea banda la BoT.
Meneja wa Idara ya Mawasiliano Benki Kuu ya Tanzania(BoT) Bi. Vick Msina akijadiliana jambo na Afisa Uhusiano kwa Umma wa benki hiyo Bi. Graciana Mahega.
Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji ameitaka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuharakisha mchakato wa kuanza kununua Dhahabu kabla ya kumalizika kwa mwaka huu ili kuwawezesha wachimbaji wakubwa na wachimaji wadogo kupata soko la uhakika.
Waziri Dkt. Kijaji ameyasema hayo leo Oktoba 8,2022 alipotembelea banda la BoT kwenye Maonesho ya 5 ya Teknolojia ya Madini yaliyofungwa leo kwenye viwanja vya EPZA Bombambili Mkoani Geita, ambapo Waziri Kijaji alikuwa Mgeni rasmi.
Dkt. Kijaji ameyasema hayo baada ya kupokea maelezo kutoka kwa Meneja Msadizi Akiba ya Fedha za Kigeni wa Benki kuu ya Tanzania (BoT) Dkt. Anna Lyimo, kuhusu mpango wa Taasisi hiyo kuanza kununua dhahabu kutoka kwa wachimbaji hapa nchini.
Dkt. Lyimo ameelezea dhamira ya BoT na wajibu wa kisheria wa kuhifadhi akiba ya fedha za kigeni hapa nchini.
“Benki kuu imefanya tafiti mbalimbali kupata vyanzo ili kuongeza akiba ya fedha za kigeni, ambapo moja ya tafiti iliyofanywa baada ya mabadiliko na maboresho katika sheria ya madini na sekta ya madini kwa ujumla ni uanzishwaji wa viwanda vya kuchenjulia dhahabu, pamoja na kukua kwa teknolojia ya kupima viwango vya dhahabu ambavyo vyote kwa pamoja vimesaidia kuongeza kiwango cha fedha za kigeni hapa nchini” ameeleza Dkt. Lyimo.
Ameongeza kwamba madini hayo yatanunuliwa hapa nchini kwa fedha za kitanzania na baadae kupelekwa nje ili kuongezewa thamani ili yaweze kuthibitishwa katika viwango vya kimataifa na kuhifadhiwa katika masoko ya kimataifa kwa kutumia fedha zetu za kigeni zilizopo nchi za nje .
Aidha amezitaja faida mbalimbali zitakazopatikana kwa kununua dhahabu nchini ikiwa ni kuongeza kiwango cha akiba ya fedha za kigeni kwa bei nafuu, pamoja na kuisaidia serikali kupunguza kiwango cha mikopo ambayo serikali ingetakiwa kukopa ili kuongeza akiba ya fedha za kigeni.
Faida nyingine ni kuipatia sekta ya madini soko la uhakika ambapo wachimbaji wadogo na wakubwa wa madini badala ya kwenda kuuza madini yao katika masoko ya nje wanaweza kwenda BoT kuuza madini yao kwa bei nzuri na ya uhakika ambapo itawapunguzia gharama za kwenda nje ya nchi.
Amehitimisha kwa kusema Benki kuu itatoa taarifa kwa wananchi kuhusu tarehe rasmi ya kuanza kununua madini ya dhahabu nchini.