Na Mapuli Misalaba, Shinyanga
Afisa ustawi wa jamii msaidizi wa Mkoa wa Shinyanga Prisla Mushi amewataka viongozi na wajumbe wanaotekeleza kampeni ya shujaa wa maendeleo na ustawi wa jamii SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga kufanya kazi kwa kuzingatia sheria,taratibu na miongozo ya serikali ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Ametoa maagizo hayo leo akiwa mgeni rasmi kwenye kikao kazi cha SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga kilichohusisha viongozi mbalimbali wakiwemo wenyeviti wa mitaa pamoja na wadau wengine.
Afisa ustawi Mushi pamoja na mambo mengine amewaagiza SMAUTAJA Mkoa wa Shinyanga kusimamia haki na kuepukana na vishawishi vya RUSHWA katika utekelezaji wa majukumu yao.
“SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga mnatakiwa kushirikiana na jamii vizuri hicho cha kwanza lakini cha pili mfanye kazi kwa kufuata sera, miongozo na sharia za kazi na utaratibu wa masuala ya ukatili lakini mshirikiane na viongozi mbalimbali muwe na mawasiliano na viongozi kingine mfanye kazi kwa kufuata haki epuka vishawishi vya RUSHWA lakini mtoe elimu kulingana na kundi lililopo”.amesema afisa ustawi Mushi
Aidha afisa ustawi huyo wa Mkoa wa Shinyanga Prisla Mushi ametaja takwimu za ukatili Mkoa wa Shinyanga kuwa ni asilimia 78 na kwamba ndiyo mkoa unaoongoza kwa ukatili Nchini Tanzania ambapo amewasisitiza SMAUJATA kuwa wapunifu ili kupunguza au kumaliza kabisa ukatili.
Mushi ametumia nafasi hiyo kuwasihi viongozi kwenda kushirikiana na jamii kwa kuwapa elimu ambapo amesema chanzo cha ukatili katika jamii ni uelewa mdogo na kwamba wengi wao hawashiriki kwenye ibada za kanisani.
“Tunatakiwa tujue kwa nini sisi ni asilimia 78 halafu kwa nini Tanga 25 kwa nini Zanziber 14 tunasema kwamba ugumu wa maisha umaskini je huo umaskini upo Shinyanga tu Tanga haupo Zanziber haupo tunatakiwa tujiulize hapo tukishajua tu ndiyo tutajua tuanzie wapi”.
“Tukimjua Mungu hatuwezi tukasema kwamba mimi kwa vile ni maskini ngoja tu nimuoze binti yangu na umri mdogo ili nipate mali kwasababu utakuwa unajua kabisa sheria na taratibu za Mungu kwahiyo huwezi kufanya ukatili huo, lakini kitu cha kufanya cha kwanza tunatakiwa tumjue Mungu na makatazo yake”. Amesema Prisla Mushi
Kwa upande wake afisa maendeleo ya jamii Mkoa wa Shinyanga Bwana Tedson Ngwale ameiomba jamii kutoa taarifa ya vitendo vya ukatili unaendeleo kufanyika kwenye familia na taasisi mbalimbali mkoani Shinyanga ili hatua zaidi za kiserikali ziweze kuchukuliwa.
Akizungumza Mwenyekiti wa Kampeni ya Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga Baraka Joseph amesema amepokea maelekezo na ushauri uliotolewa na viongozi wa serikali pamoja na wadau mbalimbali na kwamba atahakikisha SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga inaongeza ubunifu pamoja na kufanyakazi kwa kuzingatia sheria na taratibu za serikali.
Amesema SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga wamejipanga kuhakikisha wanashirikiana na jamii kuibua ukatili unaoendelea kufanyika ambapo amewaomba wananchi kuendelea kutoa taarifa za ukatili sehemu husika au kupiga namba ya bure 116 lengo ni kupunguza au kumaliza kabisa vitendo vya ukatili Mkoa wa Shinyanga.
Kampeni ya shujaa wa maendeleo na ustawi wa jamii SMAUTAJA Mkoa wa Shinyanga ambayo ipo chini ya Dkt Dorothy Gwajima waziri wa maendeleo ya jamii jinsia, wanawake na makundi maalum, imefanya kikao kazi kilichohudhuriwa na wadau pamoja na viongozi wa serikali wakiwemo maafisa ustawi wa jamii pamoja na afisa maendeo ya jamii Mkoa wa Shinyanga.