Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
NAIBU Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdala Ulega ambaye pia ni Mbunge wa Mkuranga Mkoani Pwani ameutaka Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kuhakikisha wanaondoa changamoto ya ufinyu wa barabara ya kwenda mikoa ya Kusini kwa kuipanua ipitike kwa urahisi.
Ulega aliyasema hayo alipotembelea kwenye banda la Tanroads mkoa wa Pwani kwenye maonyesho ya tatu ya wiki ya Biashara na uwekezaji yanayofanyika Maili Moja Wilayani Kibaha.
Alisema Mpango wa kuipanua barabara hiyo inayopita Mkuranga uko kwenye ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) hivyo lazima utekelezaji ufanyike.
“Mkuranga ni moja ya Wilaya zenye uwekezaji mkubwa wa viwanda kwenye mkoa wetu na wawekezaji wasingependa kupata vikwazo wanaposafirisha bidhaa au kwenda ofisini hivyo fanyieni kazi suala hilo muondoe kikwazo hicho,”alisema Ulega.
Aidha alisema kuwa changamoto hiyo ikiondolewa itaifungua Mkuranga na mikoa ya Kusini kwani uwekezaji umeanza kuelekea huko kuanzia Mkuranga, Kibiti, Rufiji na mikoa hiyo jirani ya Lindi na Mtwara.
“Tuliahidi kuwawekea mazingira mazuri wawekezaji ikiwemo kwenye suala la miundombinu ya barabara hivyo kuna haja ya kuboresha barabara zetu ikiwemo hiyo ya Mkuranga inayoelekea mikoa ya Kusini,”alisema Ulega.
Alibainisha kuwa ufinyu wa barabara hiyo kwa sasa ni changamoto kubwa kwani uwekezaji unaelekea upande huo hivyo lazima tuondoe kero hiyo ambayo inazidi kuwa kubwa kadri muda unavyosogea.
“Wawekezaji wanapenda mazingira mazuri hivyo hilo lisiwe kikwazo kwani huo ni mpango ambao upo muda mrefu kikubwa ni kufanya utekelezaji wa Mpango huo,”alisema Ulega.