Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa Tabora Dkt Peter Nyanja akizungumza na waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari Ofisi kwake.
…………………………………..
HALMASHAURI ya Manispaa Tabora imepokea fedha kiasi cha sh bil 1.38 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba 69 vya madarasa katika shule za sekondari, vyumba hivyo vinatarajiwa kutumiwa na wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka 2023.
Hayo yamebainishwa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo Dkt Peter Nyanja alipokuwa akitoa taarifa ya kupokea fedha hizo mbele ya vyombo vya habari katika ukumbi wa mikutano wa manispaa hiyo.
Alisema fedha hizo zimekuja wakati mwafaka ambapo wanafunzi wapatao 7,321 wa darasa la 7 (ke…. Me….) wameanza mitihani yao ya kuhitimu elimu ya msingi katika manispaa hiyo ambapo matarajio yao zaidi ya asilimia 95 ya watoto hao watafaulu mitihani hiyo na kuanza kidato cha 1 hapo mwakani.
Alibainisha kuwa jumla ya shule za sekondari 20 kati ya 24 zilizopo katika manispaa hiyo zitanufaika na fedha hizo kutokana na mgawanyo wa idadi ya vyumba vitakavyojenga katika kila shue, kila chumba kitagharimu sh mil 20.
Alitaja shule zitakazonufika na fedha hizo kuwa na idadi ya vyumba vitakavyojengwa kuwa ni Bombamzinga 6, Changa 5, Cheyo 2, Fundikira 4, Ikomwa 2, Ipuli 4, Isevya 3, Itetemia 3, Itonjanda 4, Kalunde 6, Kanyenye 2, Kariakoo 3, Kaze Hill 4, Lwanzali 3, Misha 5, Ndevelwa 4, Nkumba 3, Nyamwezi 2, Sikanda 3 na Tabora wavulana 1.
Dkt Nyanja alifafanua kuwa kabla ya kupokea hizo walikuwa na upungufu vya vyumba vya madarasa 79 lakini sasa Rais amewapelekea fedha za kujenga madarasa 69 hivyo kubakiwa na upungufu wa vyumba 10 tu ambavyo watavimalizia kwa fedha za mapato ya ndani.
‘Menejimenti ya halmashauri ya manispaa, baraza la madiwani na wakazi wote wa manispaa tunamshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu kwa kutuletea kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya ujenzi wa vyumba 69 vya madarasa sanjari na kutengenezwa madawati 40 kw kila darasa’, alisema.
Aidha alimshukuru kwa kuwaletea kiasi kingine cha sh bil 4.4 mwezi Septemba mwaka huu kwa ajili ya utekelezaji shughuli mbalimbali za maendeleo, ikiwemo sh mil 100 za ukarabati shule ya sekondari ya wasichana Tabora.
Aliongeza kuwa kiasi kingine kama hicho kilielekezwa shule ya msingi Gongoni kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu na sh mil 114 zilielekezwa kujenga nyumba za walimu katika shule za msingi 3.