Na Mathias Canal, WEST-Mwanza
Serikali imetumia Shilingi Bilioni 1 kwa ajili ya kukarabati na kuongeza miundombinu ya elimu ya Chuo cha Ualimu Butimba kilichopo katika Wilaya ya Nyamagana Mkoani Mwanza.
Butimba ni kati ya Vyuo vilivyonufaika na jitihada za serikali katika kuimarisha sekta ya elimu huku uongozi wa chuo hicho ukipongezwa kwa usimamizi madhubuti wa rasilimali fedha.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe Prof Adolf Mkenda ameyasema hayo tarehe 7 Octoba 2022 wakati akizungumza na Menejimenti na watumishi wa Chuo cha Ualimu Butimba wakati akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Mwanza.
Waziri Mkenda amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan kwa kuimarisha sekta ya elimu kwani muelekeo wa serikali katika kuwekeza kwenye sekta ya elimu umezidi kuimarika maradufu.
“Tusiposema watu wanasahau, Mazuri yanafanyika halafu tunasahau na muelekea wa serikali ya awamu ya sita ni kupeleka fedha nyingi zaidi kwenye miradi ya maendeleo katika Halmashauri” Amekaririwa Waziri Mkenda
Amewataka walimu na watumishi wote wa Chuo hicho kuhakikisha kuwa wanaunga mkono juhudi za serikali kwenye sekta ya elimu na shughuli zote za maendeleo huku akisisitiza kuwa changamoto katika sekta ya elimu haziwezi kukosekana lakini serikali inaendelea kuzitafutia ufumbuzi.
Waziri Mkenda ameutaka uongozi wa Chuo cha Ualimu Butimba kuhakikisha kuwa unaendelea kusimamia miradi kwa uaminifu mkubwa huku akiupongeza kwa matumizi mazuri ya fedha zote za miradi.
Kadhalika Waziri Mkenda amempongeza Mbunge wa Jimbo la Nyamagana Mkoani Mwanza Mhe Stanslaus Mabula kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya ya kuhamasisha shughuli za maendeleo katika jimbo lake hususani miradi ya elimu.