Baadhi ya madiwani wa Manispaa ya Mpanda wakipita kutoa mkono kwa Mwenyekiti wa CCM baada ya kukabidhi simu janja kwa ajili ya usajili wa wanachama.
……………………………..
Na. Zillipa Joseph, Katavi
Madiwani wa Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi wamenunua simu janja 20 zenye thamani ya shilingi milioni nne na laki nane kwa ajili ya kusajili wanachama wa chama cha mapinduzi kuanzia katika matawi, shina hadi kata kwa mfumo wa kielektroniki lengo likiwa kuimarisha kitengo hicho ili kupata idadi kamili ya wanachama wa chama hicho katika manispaa hiyo.
Akizungumza kwa niaba ya madiwani hao; Meya wa Manispaa ya Mpanda Haidary Sumri amesema licha Manispaa kuwa na kata 15 wamenunua simu 20 ili kusaidia usajili kwa kata zenye idadi kubwa ya watu.
‘Kwa kata kama Kakese, Kawajense, Nsemulwa na nyingine itakayoonekana kuwa na idadi kubwa ya watu basi hapo zitatumika simu zaidi ya moja ili kufanikisha zoezi la usajili, kama mnavyojua mtaji wa chama ni watu, kwa hiyo tumenunua simu hizi ili kuimarisha mfumo wetu wa kielektroniki na kupata idadi sahihi’ alisema Sumri.
Akizungumza mara baada ya kupokea simu hizo Katibu wa CCM wilaya ya Mpanda Sadick Kadulo amesema simu hizo zitasaidia kuongeza kasi ya usajili na kuahidi kuzitunza vizuri.
‘Baada ya hapa sasa tunakwenda kusajili kwa kasi, kwa sababu simu moja ina uwezo wa kusajili watu mia tano kwa siku, na madiwani wa Halmashauri ya Nsimbo wakifanya hivi nina uhakika tutafanya kazi vizuri zaidi’ alisema Kadulo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mpanda Method Mtepa amewashukuru madiwani hao na kusema kitendo hicho kinaashiria umoja katika chama hicho.
‘Wenzetu wamejibanabana na kukitendea haki Chama Cha Mapinduzi na kununua simu hizi, sasa na sisi tumekitendea nini Chama? Tusiendekeze maneno maneno yasiyo na msingi tufanye vitu vinavyoonekana’ alisisitiza Mwenyekiti huyo mpya wa CCM wilaya ya Mpanda