Mwanasheria wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) Anneth Mfinanga.
………………………………
Na Mwamvua Mwinyi ,Pwani
MWANASHERIA wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) Anneth Mfinanga ameshukuru mkoa wa Pwani kuandaa maonyesho ya tatu ya wiki ya biashara na uwekezaji kwani kumekuwa na mwitikio wa wafanya biashara na watu binafsi ambao wamefika kwenye banda lao .
Mfinanga amesema hayo leo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari , kwenye maonyesho hayo yanayoendelea kwenye viwanja vya stendi ya zamani ya mailimoja Kibaha Mkoani Pwani.
“Watu wengi waliojitokeza wamefanikiwa kupata vyeti vya usajili jambo ambalo linaleta hamasa” alisema Mfinanga.
“Tangu tumeanza maonyesho haya Oktoba 5 licha ya mwamko pia kuna changamoto ambazo zimejitokeza kwani wapo wafanya biashara ambao wamekuwa wakifanya biashara bila ya kujisajili na wamefika hapa ili kupata usajili “
“Wameshaanza biashara jambo ambalo tunapoingia kwenye mtandao tunakuta jina limeshasajiliwa huku mteja akilazimisha kutumia jina ambalo hajalisajili kwa sababu ya kuhofia kupoteza wateja “
Mfinanga aliwasisitiza wafanyabiashara waende BRELA kujisajili kabla ya kuanza kufanya biashara .
Amezitaja huduma wanazozitoa ni pamoja na usajili wa alama za biashara, usajili wa makampuni , usajili wa majina ya biashara, usajili wa alama za biashara usajili na utoaji wa kusajili ubunifu.