KAIMU Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho Tanzania, Francis Alfred,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Oktoba 8,2022 jijini Dodoma wakati akitoa taarifa kuhusu Utekelezaji wa Shughuli mbalimbali za taasisi hiyo na mwelekeo wa utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
Waandishi wa habari wakimsikiliza Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho Tanzania, Francis Alfred,wakati akitoa taarifa kuhusu Utekelezaji wa Shughuli mbalimbali za taasisi hiyo na mwelekeo wa utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2022/2023 leo Oktoba 8,2022 jijini Dodoma.
………………………………
Na Alex Sonna-DODOMA
KAIMU Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho nchini, Francis Alfred, amesema kuwa mwaka huu wamepanga kuzalisha tani 400,000 za korosho na mfumo utakaotumika utakuwa wa stakabadhi ghalani.
Hayo ameyasema leo Oktoba 8,2022 jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Utekelezaji wa Shughuli mbalimbali za taasisi hiyo na mwelekeo wa utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
Amesema kuwa Bodi ya Korosho nchini itashirikiana na Bodi ya Usimamizi wa stakabadhi za ghala na Tume ya Maendeleo ya Ushirika zimeandaa na kutoa Mwongozo wa Pamoja wa Usimamizi wa Masoko na Mauzo ya korosho ghafi kwa msimu 2022/2023.
Amesema Bodi ya Korosho imetoa miongozo mingine ambayo ni mwongozo wa usimamizi na udhibiti ubora wa korosho pamoja na Mwongozo wa upatikanaji wa korosho ghafi kwa wabanguaji wa ndani kupitia soko la awali kwa msimu 2022/2023.
” Miongozo yote mitatu tayari imesambazwa kwa Sekretarieti za Mikoa, Vyama vikuu vya Ushirika, Waendesha ghala, wanunuzi na wadau wengine katika mnyororo wa zao la korosho. Aidha miongozo hii inapatikana katika tovuti ya Bodi ya korosho ambayo ni www.cashew.go.tz,”amesema Bw.Alfred
Aidha amewataka wakulima katika vyama vya msingi na vyama vikuu waanze kufungua na kukusanya korosho kwenye vyama hivyo.
“Bodi ya usimamizi wa ghala waanze kufungua maghala ili wakulima wakikusanya kwenye vyama vya msingi, zipelekwe ghalani ili lengo letu la kuanza Oktoba 14, mwaka huu lifanikiwe,”amesema Bw.Alfred
Amefafanua kuwa wameweka mkakati kuhusu vifungashio vya magunia ambapo wanahitaji magunia 500,000 ili kukabiliana na tatizo la vifungashio.
Bw.Alfred amesema kuwa bodi imeanza kusajili na kutoa leseni kwa wanunuzi wa korosho ghafi kwa ajili ya kusafirisha nje ya nchi na kubangua nchini ambapo hadi kufikia tarehe 07 Oktoba, 2022, jumla ya kampuni 48 zimejisajili na kati yake, kampuni 18 tayari zimepata leseni na zilizosalia zipo katika hatua mbalimbali za kukamilisha upataji wa leseni.