Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini Mhandisi Yahya Ismail Samamba,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Oktoba 7,2022 jijini Dodoma wakati akitoa taarifa kuhusu Utekelezaji wa Shughuli mbalimbali za taasisi hiyo na mwelekeo wa utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
Waandishi wa habari wakimsikiliza Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini Mhandisi Yahya Ismail Samamba,wakati akitoa taarifa kuhusu Utekelezaji wa Shughuli mbalimbali za taasisi hiyo na mwelekeo wa utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
………………………………..
Na Alex Sonna-DODOMA
Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini Mhandisi Yahya Ismail Samamba,amesema kuwa katika vipaumbele vya bajeti ya Mwaka 2022/23, wanatarajia kukusanya Sh. bilioni 822, kusimamia ipasavyo miradi ya madini, kuimarisha zaidi hali ya usalama, afya na mazingira ya migodi.
Hayo ameyasema leo Oktoba 7,2022 jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Utekelezaji wa Shughuli mbalimbali za wakala huyo na mwelekeo wa utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
Mhandisi Samamba amesema kuwa katika mwaka huu wa fedha tume ya madini imejipanga kukusanya sh. bilioni 822 kupitia maduhuri yatokanayo na shughuli za migodi.
“Kuendelea kufungamanisha sekta ya madini na sekta zingine, kusimamia ipasavyo ushiriki wa wazawa, kuendelea kuvutia wawekezaji, kuzuia kupambana na utoroshaji na biashara haramu ya madini na kuendelea kutoa elimu kwa umma na wawekezaji,”amesema
Aidha, amesema kuwa tayari leseni tatu za uchimbaji mkubwa za madini zimetolewa na kwasasa kuna leseni moja ambayo ipo kwenye hatua za mwisho itatolewa hivi karibuni.
Kuhusu miradi ya kimkakati, Mhandisi Samamba amesema Tume imejipanga vizuri kusimamia ipasavyo miradi yote ya madini itakayozalisha nishati safi kwa ajili ya utengenezaji wa betri za magari, nishati ya kuendeshea mitambo mikubwa na madini yatakayotumika katika teknolojia kubwa.
“Matumizi ya madini yanayotumika katika teknolojia kubwa kama ndege, roketi, silaha za kisasa yameongezeka.Tume tumejianga ipasavyo kusimamia miradi yote ya madini ya Nikel, Lithium, Colbat, Graphite, Ree, Niobium, ili taifa inufaike nayo,”amesema
Amefafanua kuwa zaidi ya leseni 828 za madini hayo zimetolewa kwenye maeneo mbalimbali nchini.
Aidha amesema kuwa mchango wa sekta ya madini kwenye Pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia 4.8 Kwa mwaka 2018 hadi kufikia asilimia 7.3 mwaka 2021 lengo ni kuchangia ukuaji wa pato la taifa kwa asilimia 10 ifikapo 2025.3
“Ukuaji wa sekta ya madini mwaka 2021 ulikua kwa asilimia 9.6 ukilinganisha na ukuaji wa asilimia 1.5 kwa mwaka 2018. Aidha, jumla ya mitambo mitatu ya kusafishia dhababu imejengwa na mashine 23 za kuongeza thamani madini zimekamilika,”amesema
Mhandisi Samamba amesema tume imewezesha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kukusanya kodi mbalimbali kutoka katika migodi mikubwa ambapo kuanzia mwaka wa fedha 2019 hadi kufikia Mei, 2022 ni takriban sh. trilioni 3.77.
Amesema fedha hizo ni nje ya zile ambazo tume ilikusanya kutokana na mauzo ya bidhaa zitokanazo na madini.
“Ajira kwa wazawa katika migodi imefikia asilimia 97 ikilinganishwa na asilimia 70 iliyokuwepo mwaka 2018. Kupitia ajira hizo, watanzania wameendelea kupata ujuzi na uzoefu ili baadae miradi hii isimamiwe na watanzania kwa asilimia 100,”alibainisha
Kwa upande wake Msemaji wa serikali na mkurugenzi wa idara ya habari -MAELEZO , Gerson Msigwa,amesema kuwa malengo ya serikali ni kutanua wigo katika sekta ya uchimbaji wa madini kwa kufanya tafiti mbalimbali ili serikali inufaike kupitia sekta hiyo.
”Tanzania ni moja ya nchi ambazo zimejaaliwa na Mungu kuwa na utajiri mkubwa wa madini, tunachokifanya ni kutafiti kufahamu yalipo ili yaweze kunufaisha nchi, katika kutekeleza hili tunashirikiana na sekta binafsi.”amesema Bw.Msigwa