Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
Mfuko wa Taifa wa hifadhi ya jamii (NSSF) Mkoani Pwani ,umetoa fursa kwa wawekezaji, wafanyabiashara , wateja na jamii kijumla kununua viwanja ambavyo imetenga kwa ajili ya uwekezaji na makazi.
Akielezea umuhimu wa kushiriki katika maonyesho ya tatu ya wiki ya biashara na uwekezaji Mkoani Pwani yanayofanyika Mailmoja Kibaha Mjini, meneja wa NSSF Mkoani Pwani,Witness Patrick alieleza, wameweka banda lao ambapo kila mmoja akifika ataweza kuelezwa namna ya kupata Raslimali ya ardhi ili kuinua maendeleo na uchumi.
Aliwajulisha wawekezaji watambue kuwa kuna viwanja vya ukubwa mbalimbali na vipo kwenye Mazingira ya uwekezaji.
Pia Witness alifafanua kwamba, ipo sheria inayowataka wawekezaji kuwaunganisha wafanyakazi wao katika mfuko huo ,hivyo amewataka waajiri, wawekezaji kuwaunganisha wafanyakazi wao katika mfuko.
Katika hatua nyingine, meneja huyo alitoa wito kwa waajiri kulipia michango Yao kwa wakati ili kuondoa usumbufu.
Hayo aliyasema wakati wa maadhimisho ya kilele Cha wiki ya NSSF mkoani hapo ambapo walisheherekea pamoja na watumishi na wateja walipofika kupata huduma.
Alihamasisha walio kwenye sekta zote za binafsi na sekta rasmi kujiunga na mfuko wa NSSF ili kunufaika na mafao ya mfuko huo.
“Wiki hii ni muhimu Sana kwetu inatupa nafasi ya kuwatambua wateja wetu kwani wao ni bora kwetu na kuwatambua watumishi wetu kwa kutoa huduma bora kwa wateja”alifafanua Witness.
Kwa upande wa wanachama wa NSSF waliofika kupatiwa huduma akiwemo Linus Mhina na Mary Nchimbi waliipongeza NSSF Pwani kwa huduma bora na kutoa elimu kwa wanachama wao.
Mary alisema , kwasasa NSSF haina usumbufu Kama ilivyokuwa kipindi cha nyuma ambako mafao ulikuwa unacheleweshewa hulipwi hadi unakufa .
“Na sisi wanachama tuwaunge mkono ,tumekuwa tukitaka huduma ya haraka wakati wenzetu wanafuata Sheria na taratibu zao “alieleza Mary.
Nae Mhina alielezea ,huduma zimerahisishwa kwa waajiri na wafanyakazi kwa Sasa wanalipa na kutuma vyote wanavyojaza kwa njia ya kielektroniki bila kufika ofisini.