Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango akiwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Dkt. Khatibu Kazungu, kabla ya ufunguzi wa Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali na Mikoa (SHIMIWI) 2022, jijini Tanga.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bi. Jenifa Omolo, akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa michezo wa wizara hiyo katika Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali na Mikoa (SHIMIWI) 2022, jijini Tanga.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Jenifa Omolo, akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa wizara hiyo wanaoshiriki katika Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali na Mikoa (SHIMIWI) 2022, jijini Tanga.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WFM, Tanga)
***********************
Na. Saidina Msangi, WFM, Tanga
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bi. Jenifa Omolo, amewataka Watumishi wa wizara hiyo kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi ili kujiweka sawa kiafya na pia kuweza kushiriki katika michezo kikamilifu.
Bi. Omolo ametoa wito huo wakati akizungumza na watumishi wa wizara hiyo wanaoshiriki katika Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali na Mikoa (SHIMIWI) 2022 yanayoendelea jijini Tanga.
‘’Nimefurahia maendeleo yenu katika michezo hii lakini niwakumbushe viongozi kuhimiza watumishi kufanya mazoezi, kuandaa mechi za kirafiki ili kujiweka sawa kwa mashindano kama haya’’ alisisitiza Bi. Omolo.
Alisema kuwa ana imani na ushiriki wa timu za Wizara ya Fedha na Mipango katika michezo hiyo inayoendelea japo kuwa kuna kushinda na kushindwa huku akiwatakia kila la heri na ushindi katika michezo hiyo inayoendelea kwa siku 14.
Bi. Omolo alipongeza timu za Wizara ambazo zimehusisha watumishi kutoka Tanzania Bara na Zanzibar kwa hatua waliyofikia na kuwajulisha kuwa Wizara itaendelea kuwa pamoja nao kuhakikisha kuwa wanashiriki michezo hiyo kikamilifu.
Mashindano ya Shimiwi kwa mwaka huu yenye kauli mbiu ‘’michezo hupunguza magonjwa yasiyoambukiza na kuongeza tija mahala pa kazi’’, yanafanyika kwa siku 14 ambapo michezo mbalimbali ikiwemo kuvuta kamba, mpira wa miguu, mpira wa pete pamoja na bao inatarajiwa kuchezwa na timu zinazoshiriki michezo hiyo.