************
Na.Catherine Sungura,WAF-Misenyi
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu ameagiza kupelekwa kwa vifaa tiba ikiwemo mashine ya usingizi na upasuaji ndani ya wiki moja kwenye kituo cha afya cha Kabyaile kilichopo kata ya Ishozi Wilayani Misenyi ambacho kimebainishwa kama kituo maalumu cha matibabu kwa wagonjwa watakaopatikana na ugonjwa wa Ebola.
Waziri Ummy ametoa agizo hili wakati alipofanya ziara katika kituo hicho na kuonga huku akijibu maswali kutoka kwa wakazi wa kata ya Ishozi waliofika kwenye kituo cha afya cha Kabyaile.
Amesema kwamba watatekeleza maelekezo yote yanayotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tamzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kuahidi kwamba watayasimamia maelekezo yote yanayotolewa.
“Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia kwa upande wa huduma za afya inajikita kwenye ubora wa huduma hivyo vifaa tiba tutaleta maana yake atakapotokea mgonjwa wa Ebola na anatakiwa kufanyiwa upasuaji tutafanya tutampe wapi.” Alihoji Waziri Ummy.
Hata hivyo Waziri Ummy allmemwagiza mwakilishi wa Katibu Mkuu kufuatilia oda ya vifaa tiba hivyo kwenye Bohari ya Dawa (MSD) imeenda lini na kama kweli wameoda vifaa hivyo walivyo vitaja.
Kwa upande wa Bima ya Afya kwa wote (UHC), Waziri Ummy aliwahimiza wananchi kukata bima ya afya ambayo itawaondolea gharama za matibabu na malalamiko ya kuchangia huduma za tiba pindi wanapougua.
“Bima ya afya kwa wote itatuondolea malalamiko haya ya kuchangia,hatutampiga faini mtu yeyote bali tutawahamasisha kila mtanzania kuwa na bima ya afya”.
Aidha, Waziri Ummy amewataka watumishi wa afya hususani viongozi kusema ukweli kwamba dawa hazipo na hivyo kuwataka kuboresha huduma katika vituo vyao ili kuweza kutatua changamoto zilizopo na kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya ikiwemo dawa na vifaa tiba.
Vilevile Waziri Ummy hakuacha kutoa elimu kwa wakazi hao kuhusu tishio la ugonjwa wa Ebola na kuwakumbusha wananchi hao kuendelea kuchukua tahadhari zote za kinga ikiwemo kunawa mikono mara kwa mara kwa maji tiririka na sabuni,kuepuka kugusa damu,matapishi,kamasi,mate,machozi,mkojo,kinyesi na majimaji mengine yanayotoka mwilini mwa mtu mwenye dalili za Ebola.