Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo Tnzania (BMT) Neema Msitha (wan ne kutoka kulia) wakionyesha ishara ya mshikamano wakati wa uzinduzi wa mashindano ya kanda ya tatu ya Afrika yaliyopangwa kufanyika nchini mwezi ujao kwa kushirikisha jumla ya nchi 25.
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam. Tanzania imepewa nafasi ya kuandaa mashindano ya kuogelea ya kanda ya tatu ambayo yatashirikisha waogeleaji mbalimbali kutoka nchi 25.
Mashindano hayo yamepangwa kuanza Novemba 15 mpaka 20 kwenye bwawa la kuogelea la klabu ya Gymkhana huku Tanzania ikiwa mwenyeji kwa mara ya pili katika historia.
Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya mashindano wa Chama Cha Kuogelea Tanzania (TSA), Hadija Shebe alizitaja nchi hizo kuwa ni
Burundi, Djibouti, Eritrea, Ethiopia, Kenya, Rwanda, Somalia, Sudan, Sudani Kusini, Uganda na Tanzania kwa nchi za kanda ya tatu Afrika.
Nchi za kanda ya Nne Afrika ambazo zinatarajia kushiriki katika mashindano hayo ni Angola, Botswana, Comoros, Lesotho, Madagasca, Malawi na Afrika Kusini.
Pia kuna nchi za Mauritius, Msumbiji, Namibia, Shelisheli (Seychelles), Zambia, Eswatini na Zimbabwe.
Alisema kuwa wanatarajia kuwa na wachezaji na maofisa mbalimbali zaidi ya 300 na kuwaomba wadau kusaidia kudhamini mashindano hayo makubwa ya kuogelea barani Afrika.
“Tumepewa heshima kubwa kuandaa mashindano haya na Shirikisho la Mchezo wa kuogelea la Afrika na hivyo tunaomba wadau kutusaidia ili kufanikisha mashindano haya,” alisema Shebe.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Tanzania (BMT), Neema Msitha alisema kuwa ujio wa timu zote hizo ni heshima kwa nchi na kuwaomba wadau kusaidia kudhamini.
“Naipongeza TSA kwa kupewa heshima kubwa ya kuandaa mashindano haya. Ni faraja kwa nchi kwani mbali ya kuitangaza nchi, pia inatoa fursa kwa wachezaji wetu kupima viwango vyao kimataifa na vile vile kuutangaza utalii wan chi,” alisema Msitha.
Alisema kuwa serikali ipo pamoja na TSA kuhakikisha mashindano hayo yanafianikiwa pamoja na ukweli kuwa wanahitaji msaada kutoka kwa wadhamini mbalimbali.
Kwa upande wake, meneja msaidizi wa timu ya kuogelea ya Tanzania, Asha Gomile alisema kuwa waogeleaji wa Tanzania kwa sasa wapo katika maandalizi kuelekea mashindano hayo na wanatarajia kufanya vyema.
Asha maarufu kwa jina la Mama Natalia alisema kuwa wanatarajia kufanya vyema katika mashindano hayo kama ilivyokuwa mwaka 2017 ambapo walitwaa ubingwa katika mashindano yaliyofanyika hapa nchini.
“Waogeleaji wetu wapo tayari na ikumbukwe mwaka uliopita, tulimaliza katika nafasi ya pili kaika mashindano yaliyofanyika nchii Uganda. Tupo tayari kwa mapambano na tunarajia kufanya vyema,” alisema Gomile.