Mwakilishi kutoka Benki ya Dunia (WB) Bi. Innocent Mulindwa (wa kwanza kushoto) akifafanua jambo wakati wa ziara katika kampuni ya RiversBank Fish Farm Wilayani Rungwe
Mkurugenzi wa Kampuni ya RiversBank Fish Farm Pius Nyambacha (mwenye kofia) akifurahia jambo na ujumbe uliofanya ziara katika mashamba yake ya kufugia samaki
Wajumbe kutoka Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Mamlaka ya Elimu Tanzania na Benki ya Dunia (WB) wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa kampuni ya RiversBank Fish Farm
************************
Mafunzo ya Kuendeleza Ujuzi yanayotolewa kupitia ruzuku ya Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF) unaoratibiwa na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) yametengeneza fursa za ajira kwa mamia ya vijana na akinamama katika wilaya ya Rungwe, Mkoani Mbeya kupitia mradi wa kufuga samaki.
Mkurugenzi wa shamba la kufugia samaki la RiverBanks Fish Farms, Pius Nyambancha ambalo ni miongoni mwa taasisi zilizofadhiliwa na SDF amebainisha hayo alipozungumza na wawakilishi kutoka Benki ya Dunia (WB) ambao ni wafadhili wa Mradi wa Kuendeleza Ujuzi (SDF) na viongozi kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mamlaka ya Elimu Tanzania (TE).
Amesema ruzuku ya SDF imemwezesha kufuga samaki kitaalam ikiwa ni pamoja na kumpa uwezo wa kuzalisha vifaranga hivyo kumwongezea uzalishaji ambapo katika kipindi cha miezi tisa amezalisha kilo 600 za samaki na hivyo kujiongezea kipato.
Kupitia ruzuku ya SDF, Kampuni ya RiverBanks Fish Farms ilipata ufadhili wa Shs. Milioni 131.2 ambazo zimewezesha uboreshaji wa miundombinu ya uzalishaji vifaranga vya samaki, ufugaji wa kisasa, ununuzi wa vifaa vya kisasa vya ufugaji pamoja na kuendesha mafunzo kwa vijana na akina mama 427 Wilayani Rungwe.
Nyambacha ameongeza kuwa, baada ya kujengewa uwezo na SDF amefanikiwa kutengeneza ajira kwa watanzania 726.
Wawakilishi kutoka Benki ya Dunia (WB) na viongozi kutoka Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia pamoja na TEA na wako mkoani Mbeya kwa ziara ya siku nne ya ukaguzi wa miradi katika taasisi zilizonufaika na ufadhili wa SDF