Mtendaji mkuu wa Dawasa Injinia Cyprian Luhemeja alipotembelea katika Banda hilo la Dawasa.
***********************
Na Victor Masangu,Pwani
Mamlaka ya maji Safi na usafi wa mazingira (DAWASA) imeahidi kuendelea kuboresha na kufikisha huduma ya maji kwa wawekezaji mbali mbali wa viwanda vidogo na vikubwa lengo ikiwa ni kuunga mkono juhudi za serikali katika kukuza uchumi kupitia sekta ya viwanda.
Hayo yamebainishwa leo na mtendaji mkuu wa Dawasa Injinia Cyprian Luhemeja wakati akitoa taarifa kwa Rais mstaafu wa awamu ya nne Dkt Jakaya Mrisho Kikwete alipotembelea Banda la Dawasa wakati wa ufunguzi rasmi wa maonesho ya tatu ya uwekezaji na biashara Mkoa wa Pwani.
Alisema kwamba lengo lao kubwa ni kuweza kuboresha zaidi huduma ya maji kwa wananchi wote wa Mkoa wa Dar es Salaam pamoja na Pwani ikiwemo wawekezaji wa viwanda vyote kuwapatia huduma ya maji.
“Tumeshiriki katika maonesho haya kwa lengo la wananchi waweze kufahamu utekelezaji wa majukumu yetu mbali mbali ambayo tumekuwa tukiyafanya katika mikoa ya yetu ya Dar es Salaam pamoja na Pwani na tunawahidi kuwaboreshea huhuma ya maji kuanzia ngazi za vitongoji,”alisema Luhemeja.
Aidha Luhemeja amesema kuwa hakuna tatizo la maji kutokana na mitambo yote ya ruvu chini pamoja na ule wa ruvu juu yote inafanya kazi vizuri na kwamba wameshakukua tahadhari endapo kama kukitokea na ukame.
Kadhalika alisema miradi mbali mbali kwa ajili ya usambazaji wa maeneo tofauti bado kazi inaendelea ikiwemo Sambamba na kuchimba mabwawa ambayo yatasaidia kwa kiasi kikubwa katika kipindi cha ukame wa mvua.
Kwa upande wake Rais mstaafu wa awamu ya nne Dkt Jakaya Kikwete aliupongeza Mkoa wa Pwani kwa kuandaa maonesho hayo ambayo yataweza kutoa fursa ya wafanyabiashara kuonesha bidhaa wanazozizalisha.
Kadhali alimpongeza mtendaji mkuu wa Dawasa kwa kuweza kuendelea kuwahudumia wananchi katika kuwasambazia maji safi na salama ili wananchi waweze kuondokana na changamoto ya upatikanaji wa maji.