Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
RAIS Mstaafu wa awamu ya nne ,Dkt.Jakaya Kikwete anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa wiki ya maonyesho ya Biashara na Uwekezaji Mkoani Pwani, octoba 6 mwaka huu,katika viwanja vya stendi ya zamani Mailmoja.
Aidha maonyesho hayo yatanyika kuanzia octoba 5-10 mwaka huu ,ikiwa ni maonyesho ya tatu tangu kuanzishwa kwa maonyesho hayo mwaka 2018.
Akizungumza na waandishi wa habari maandalizi ya maonyesho yalipofikia Mkuu wa mkoa wa Pwani alhaj Abubakari Kunenge, alisema washiriki na wawekezaji waliothibitisha kuwepo ni 200 na matayarisho yamefikia asilimia 95 kukamilika.
“Tunashirikiana na Shirika linalohudumia viwanda vidogo vidogo( SIDO )Kanda ya Mashariki na TANTRADE wanashughulika na uratibu “alifafanua Kunenge.
Hata hivyo,mkuu huyo wa mkoa alisema kutakuwa na kongamano la uwekezaji octoba 8 mwaka huu ,litakalofanyika chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere kilichopo Kwamfipa, Kongamano ambalo litaonyesha fursa za viwanda na uwekezaji Mkoani Pwani
“Rais Samia Suluhu Hassan anaendelea kuweka msukumo katika kuvutia wawekezaji nchini,Na tukio hili linakwenda kutafsiri kwa vitendo namna tunavyounga mkono juhudi za Serikali”alifafanua Kunenge.
Kwa upande mwingine alibainisha mkoa wa Pwani umetenga Kongani kwa ajili ya viwanda ,na maeneo ya kujenga viwanda pamoja na kuboresha miundombinu mbalimbali ili kuwaondolea changamoto wawekezaji.
Kunenge alitaja malengo ya maonyesho na kongamano hilo ,Kuwa ni pamoja na kuunga mkono juhudi za Serikali kupitia Rais Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha wanainua sekta ya viwanda na uwekezaji, wananchi kuona bidhaa zinazozalishwa Mkoani humo na na kuinua soko la wawekezaji.
“Hakuna urasimu katika maonyesho haya ,nitoe rai kwa wawekezaji na wafanyabiashara kujitokeza kushiriki ili kuja kujitangaza na tumejipanga kuna mabanda , ulinzi wa kutosha pamoja na miundombinu mizuri”
Akizungumzia sekta ya kilimo , aliwahimiza wakulima wa mazao mbalimbali kulima kwa tija ili wawekezaji wa viwanda vya kusindika na wa mazao Kama matunda waone ipo chachu ya kuwekeza katika hilo.
Kunenge alieleza kwamba , upande wa utalii jitihada za kijitangaza kimkoa upo mpango maalum baina ya mkoa na Wizara ya utalii kuja kufanya ziara ya kutembelea vivutio vyote 72 vilivyopo Mkoani hapo kwa lengo la kuweka mikakati ya namna ya kujitangaza zaidi ndani na nje ya nchi.
Nae mama lishe MariaFord ,aliishukuru Serikali na Rais Samia na mkoa kwa kuona mamalishe ni sehemu ya wafanyabiashara ambao wanapaswa kupata fursa ya kujiongezea kipato.
“Hii ni fursa ya kipekee haijawahi kutokea maana tumeshirikishwa na mmeshuhudia hapa mkuu wa mkoa katupatia kiasi cha sh.milioni moja ili kujenga vibanda vyao kwenye maonyesho hayo na waweze kushiriki Kama wengine”alifafanua.
Diwani wa kata ya Mailmoja, Ramadhani Lutambi aliwaomba wananchi kujitokeza kushiriki maonyesho hayo na kujitoa Kama ilivyo katika maonyesho ya sabasaba na nanenane.
Lutambi alisema ni,fursa kubwa kwa wafanyabiashara na Taasisi mbalimbali kutumia mwanya huo kujitangaza kwenye jamii .
Mwenyekiti wa wamachinga Mkoani Pwani, Philemon Maliga alielezea ,watajifunza kupitia wawekezaji wakubwa nanma ya kuzalisha ,kujitangaza,kupata masoko na watakuwa wadau kutokana na kuondoka katika kujitegemea kutoka walipo na kuwa wawekezaji wakubwa na kuanzisha viwanda japo vidogo.