***********************
Na Mwandishi wetu, Babati
MKUU wa Wilaya ya Kigoma, Ester Mahawe amechaguliwa kuwa Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa kupitia Wilaya ya Babati Mjini Mkoani Manyara.
Msimamizi wa uchaguzi huo, ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Mkoa wa Manyara, Fratern Kwahhison ndiye ametangaza matokeo hayo.
Kwahhison amesema nafasi ya kwanza imeshikwa na Elias Iyo ambaye ameongoza kwa kupata kura 225.
Amesema Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Ester Alexander Mahawe ameshika nafasi ya pili kwa kupata kura 206.
Kwahhison amesema Emmanuel Khambay ameibuka mshindi wa tatu kwa kupata kura 174.
Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Mahawe akizungumza baada ya matokeo hayo kutangazwa amewashukuru wajumbe hao kwa kumchagua kwenye nafasi hiyo.
“Kwa dhati ya moyo wangu nawashukuru mno kwa heshima hii kubwa mliyonipatia na kunichagua kwa kishindo kushika nafasi hii,” amesema Mahawe.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya wazazi Mjini Babati Emmanuel Khambay akizungumza baada ya matokeo amewashukuru wajumbe hao kwa kumchagua kwa kura hizo 174.
“Imani huzaa imani, nawashukuru mno kwa wajumbe kuzidi kuniamini na kunipa kura ambazo zimesababisha mimi kupata nafasi hiyo, natoa ahadi ya kuwawakilisha vyema,” amesema Khambay.
Pia, Kwahhison amemtangaza Elizabeth Marley kuwa ameweza kutetea nafasi yake ya Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Babati Mjini, baada ya uchaguzi huo uliokuwa na ushindani mkali kurudiwa mara mbili.