Na. Zillipa Joseph, Katavi
Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi, Wilaya ya Mpanda mkoani Katavi wamemchagua Method Mtepa kuwa Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Mpanda baada ya kuongoza kwa kupata kura 532 na kuwashinda Emanuel Manamba aliyepata kura 150 na Mweji Kabudi aliyepata kura 150.
Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo uliofanyika katika uwanja wa Azimio, Msimamizi Mkuu wa Uchaguzi wilaya ya Mpanda Mwl. Joseph Lwamba amesema jumla ya kura zote zilizopigwa ni 852 ambapo kura 20 ziliharibika.
“Kwa mamlaka niliyopewa,naomba rasmi nimtangaze Method Philip Mtepa kuwa ndiye mwenyekiti wetu wa CCM Wilaya ya Mpanda” amesema
Mwl. Lwamba amesema wanachama waliopaswa kufika katika mkutano huo ni 1226 lakini kutokana na sababu mbalimbali wengine hawakuweza kufika.
Aidha katika uchaguzi huo Elias Mwanisawa amechaguliwa kuwa katibu wa itikadi, siasa na uenezi wilaya ya Mpanda baada ya kupata kura 81dhidi ya mshindani wake Gilbert Kaswiza aliyepata kura 48.
.
Akishukuru wanachama Mtepa amesema huu ni wakati wa kuongoza kwa ushirikiano na kuwataka wanachama wa chama hicho kutosita kwa ushauri wowote.
“Sikuchaguliwa ili nije nikorofishane na wana CCM,hicho kitu sitaki. nikikosea niambieni oya dogo hapa umekosea”alisema Elias Mwanisawa,mshindi wa nafasi ya Katibu wa itikadi,siasa na uenezi Wilaya ya Mpanda.
Hata hivyo,katika uchaguzi huo wajumbe wamewachagua wajumbe 10 wa Halmashauri Kuu ya Wilaya wakiwemo wajumbe 3 wa mkutano mkuu wa Mkoa.
Awali Mwenyekiti aliyemaliza muda wake Abel Kimanzi ametoa wito kwa viongozi waliochaguliwa kudumisha umoja, upendo na mshikamano ili kuendeleza mafanikio waliyopata.